Makala

NGILA: Bila ushirikiano kiteknolojia #AfricaRising itasalia ndoto tu

September 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na FAUSTINE NGILA

RIPOTI ya hivi majuzi kuhusu uchumi wa dijitali iliyochapishwa na Umoja wa Mataifa (UN) imetoa takwimu za kushtua. Afrika huchangia chini ya asilimia moja ya mapato kutokana na biashara za kidijitali duniani!

Utafiti huo ulionyesha kuwa ni mataifa manne tu barani yanayotilia mkazo haja ya kuwekeza zaidi katika mifumo ya kidijitali –Kenya, Misri, Afrika Kusini na Nigeria – ingawa katika jukwaa la kimataifa juhudi hizo zimemezwa na Amerika na Uchina.

Hata hivyo, nikiwahoji wataalamu wa uwekezaji wa teknolojia kutoka Afrika Kusini kwa njia ya simu, nilibaini kuwa bado kuna nafasi nyingi mno kwa mataifa ya Afrika kujinyanyua na kupunguza uchochole kupitia ubunifu wa kuwekeza kwa mbinu za kisasa.

Mkuu wa kampuni ya Mastercard barani Afrika, Bw Raghav Prasad alisema Afrika imepiga hatua kubwa kwa kuwa mataifa mengi sasa yanafikiria kidijitali yanapounda sera zao za maendeleo.

“Katika miaka kumi ijayo, bara hili litakuwa limepunguza pengo lililopo kati ya matajiri na watu maskini na kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira. Gharama ya intaneti inazidi kupungua na hii ni fursa nzuri kwa Afrika kujiinua kiuchumi,” aliniambia.

Naye Bw Bhaskar Chakravorti ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tufts kinachonoa vijana katika ulingo wa uwekezaji wa kisasa, alisema Afrika imejaliwa vipaji vya kutosha ambavyo vikikuzwa ipasavyo vitaboresha maisha ya usoni.

Licha ya wataalamu hawa kudhihirisha imani yao katika kuwekeza barani Afrika, kati ya mataifa 52, ni mataifa manne tu yanayotambua umuhimu wa kuvumisha uchumi kwa kuzingatia teknolojia katika kila sekta.

Yako wapi mataifa mengine 48? Halitakuwa jambo la busara kwa Waafrika kujitapa mitandaoni wakitumia kaulimbiu na hashtegi #AfricaRising huku karibu bara zima likisalia nyuma katika teknolojia za kisasa.

Bw Prasad na Bw Chakravorti wamejawa na matumaini, lakini ili bara hili liondoe aibu ya kuchangia asilimia finyu katika soko la kidijitali kimataifa, mataifa yote yanafaa kwenda kwa kasi sawa.

Iweje mataifa kama Madagascar na Mali yawe yakisoma jinsi Kenya imekuwa ‘Amerika’ ya Afrika? Wataalamu kutoka mataifa yenye maono kama Misri, Nigeria, Afrika Kusini na Kenya wanafaa kusambaza fikra za kisasa katika mataifa yaliyoachwa nyuma ili bara hili liwe na usemi wa maana kimataifa.

Ili kubadilisha taswria ambazo zinachochea mabara mengine kudunisha Afrika, mataifa yote 52 yanafaa kushirikiana katika juhudi za kuunda mifumo ya teknolojia itakayoboresha sekta za elimu, afya, mawasiliano, uchukuzi, viwanda, utalii, kawi, kilimo, fedha, maji na ardhi.