NGILA: Dunia isipodhibiti teknolojia za #Deepfake, itaangamia
Na FAUSTINE NGILA
Wakati afisa mkuu mtendaji wa kampuni za Amerika, Tesla na Space X, Bw Elon Musk (pichani) alipotoa hotuba kuhusu haja ya kudhibiti teknolojia za kiotomatiki (AI) mwaka jana, dunia ilimpuuza.
Mwanateknolojia huyo alionya kuwa AI inatumiwa kuunda programu hatari kwa maisha ya binadamu kwa kasi mno, na hii itafanya dunia iwe sayari hatari.
“Tunahitaji udhibiti wa kipekee kuhakikisha programu za AI zinaundwa na watu waliohitimu, wanaoelewa athari zake ili kuhakikisha mazingira yake ni salama.
“Hatari inayoletwa na AI inazidi ile ya zana za kinuklia. Hakuna taifa litakaloruhusu raia wake kuunda mabomu ya kunuklia bila sheria mwafaka. Mbona sheria hizi hatuzioni kwa AI,” alishangaa.
Na kama alivyobashiri Bw Musk, wiki iliyopita programu ya simu kutoka China kwa jina Zao ilipakuliwa na watu wengi zaidi duniani, kutokana na uwezo wake wa kugeuza sura za watu kwenye filamu na video.
Teknolojia hiyo – Deepfake- Ina uwezo wa kuchukua uso wako na kuutia kwa mwili wa mwanamitindo, mwanasiasa, mwanahabari, mwigizaji, mchezaji au mtu yeyote unayetaka.
Unaweza kuipata katika Google Playstore kwa simu za Android au Apple Appstore kwa simu aina ya iPhone.
Kama tu teknolojia iliyosambaa mno katika mtandao wa kijamii wa Facebook, FaceApp, apu ya Zao inatia usiri wa watumizi katika hatari ya kudukuliwa.
Teknolojia hizi zilizokosa udhibiti sasa zimekuwa tishio kwa taaluma ya uanahabari, kwani sasa unaweza kutia maneno katika kinywa cha mtu yeyote maarufu na kueneza habari feki mitandaoni.
Hata hivyo, kampuni ya Momo inayounda programu ya Zao haifai kushutumiwa.
Wa kuelekezewa lawama ni kampuni ya Google inayoruhusu programu mbalimbali zenye uwezo wa kuhariri uso na sauti ya mtu, kuendelea kupatikana katika seva zake.
Inafaa kuzifuta na kuzizima zisionekane tena.
Hii ni kwa sababu duniani kote, hakuna sheria madhubuti za kudhibiti teknolojia hatari kama hizi, na hivyo kwa kuwa Google inamiliki asilimia kubwa zaidi ya matini kwenye intaneti, inafaa kukubali jukumu la kuwalinda walimwengu dhidi ya uvumbuzi unaolenga kuchimbua taarifa za siri huku ukieneza uvumi.
Pia mataifa tajika katika uvumbuzi wa teknolojia inayowezesha watumizi kuhariri sehemu za mwili za watu maarufu kama Uchina, Amerika na Urusi yanafaa kuweka sheria na adhabu kali kwa watu wanaochafua mitandao.
Dunia isipodhibiti teknolojia za #Deepfake itaangamia.
Huenda teknolojia hiyo haijasambaa sana hapa barani Afrika, lakini uwezo wake wa kuzua ghasia wakati video za uwongo za mwanasiasa akisema jambo la kukera mitandaoni, ni mkubwa na haufai kupuuzwa.