NGILA: Teknolojia inayoua wanadamu yafaa kukomeshwa
NA FAUSTINE NGILA
KWA mara ya pili chini ya miezi sita, ndege aina ya Boeing 737 MAX 8 ilianguka dakika chache baada ya kupaa angani na kuua watu 157 Ethiopia.
Oktoba mwaka uliopita, watu 189 waliangamia kwenye aina sawa ya ndege nchini Indonesia. Kiufundi, lazima kuna tatizo katika aina hii ya ndege inayosababisha maafa miezi michache baada ya kununuliwa.
Huku familia zikizidi kuomboleza jamaa na marafiki waliopoteza maisha, maswali yameibuka upya kuhusu usalama wa aina hiyo ya ndege, ambayo ni muhimu kwa Amerika katika mipango yake ya teknolojia ya angani.
Kutokana na hili, mataifa ya Uchina, Indonesia, Singapore, Australia, Brazil, Argentina, Mexico na Ethiopia yamechukua hatua muhimu ya kusitisha usafiri kwa aina hiyo ya ndege kwa kuwa usalama wake umejaa shaka.
Uchunguzi wa mapema kutoka kwa tovuti ya Sweden wa kufuatilia ndege zote angani, flightradar24, imefichua kuwa ndege hiyo aina ya Boeing 737 MAX 8 ilikosa udhibiti wakati wa kupaa.
Ajali ya Indonesia pia ilitokea dakika chache baada ya kupaa, huku uchunguzi zaidi ukionyesha kuwa ndege hiyo ina programu ya ambayo haipo kwa aina zingine za ndege, ambayo huwatatiza marubani.
Programu hiyo mpya inafaa kusaidia ndege hiyo kupaa bila tatizo, lakini wakati wa ajali ya Indonesia, ilikuwa inailazimisha ndege kwenda chini kila mara licha ya juhudi za rubani kuisitiri hewani.
Baada ya ajali hiyo, kampuni ya Boeing ilituma ilani ya dharura ikionya marubani kuhusu tatizo katika programu hiyo, huku ikiahidi kuunda programu nyingine ya kuondoa tatizo hilo.
Ingawa siwezi kusema kuwa programu hiyo ndicho kiini cha ajali ya Ethiopia, kwa kuwa makosa ya kibinadamu pia huchangia kwa ajali, teknolojia ambayo inaletea wanadamu maafa inafaa kuondolewa kwa vifaa vinavyonunuliwa kwa matumizi ya watu, hasa usafiri.
Ninatambua kuwa teknolojia ni nguzo kuu ya maendeleo ya kila taifa, lakini iwapo uvumbuzi au utekelezaji wake una shaka, basi teknolojia hiyo inafaa kurudishwa jikoni na kuundwa vyema kwa kuzingatia usalama wa wanadamu, wanyama na mazingira.
Kampuni ya Boeing yaweza kuomba radhi kwa vifo vya watu 346 ambao waliangamia kwa ndege iliyounda, lakini haiwezi kuwafufua watu hao, wala kuzipatia familia zilizotegemea watu hao matumaini mbadala kwa maisha ya usoni.
Ni jambo la busara kwa wavumbuzi kuwa makini zaidi wanapotengeneza teknolojia ya kutumika na wanadamu, kwa kuzingatia usalama wake katika nyanja zote za maisha.