NGILA: Teknolojia itumiwe kuwapa tumaini watoto wa wakimbizi
NA FAUSTINE NGILA
WIKI iliyopita Mfumo wa Kimataifa wa Miungano ya Mawasiliano (GSMA) na kampuni ya mawasiliano ya Vodafone zilidhihirisha jinsi teknolojia inavyoweza kutumiwa kuhamasisha jamii kuhusu haki za watoto.
Kwa kuzindua mradi wa mPower Youth, mashirika haya yanapiga jeki juhudi za Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) kwa kuwapa watoto katika kambi za wakimbizi nafasi ya kupata elimu.
Mradi huo unahusisha shule za kidijitali ‘ndani ya katoni’. Hii inamaanisha kuwa kila mtoto anaweza kufaidika kutokana na mradi huo unaowapa mawimbi ya intaneti, tableti, projekta, spika na matini ya kujielimisha.
Baada ya kutambua kuwa watoto katika kambi nyingi hawawezi kupokea mafunzo ya maana kama wenzao katika jamii zilizostawi, mashirika hayo yalizindua mradi huo wa kidijitali kuinua usawa katika jamii. Kongole kwao!
Tayari kuna shule 36 katika kambi nane za wakimbizi humu nchini, Tanzania na DRC ambazo zinawafaidi wanafunzi 86,000 wanaofundishwa na walimu 1,000.
Mradi huo pia utawashughulikia wanafunzi kiafya, pamoja na kuwalinda dhidi ya dhuluma na maafa kutokana na mafuriko huku ukiwasaidia kupata chakula cha kutosha.
Hii inaashiria jinsi licha ya Afrika kuwa na watu wabunifu, serikali katika bara hili zimezidi kuchangia kwa utovu wa usawa katika utoaji wa huduma za kimsingi kama elimu, afya, chakula na usalama, ambazo ni haki za kila mtoto.
Kuna jumla ya wakimbizi milioni 25.9 duniani katika kambi mbalimbali, na zaidi ya nusu ni watoto.
Ingawa serikali za mataifa yenye wakimbizi yanatambua hili, zimezembea kuwapa watoto haki zao za kimsingi kama wananchi wake.
Kuna mtindo hapa Afrika wa kuwabagua wakimbizi ni kana kwamba si binadamu eti kwa sababu walitoroka mataifa yao. Hali hii yafaa kukoma kwani machoni pa Mola, watu wote ni sawa.
Kenya, kwa mfano, inaelewa zaidi uwezo wa teknolojia katika kusuluhisha changamoto za kijamii kama wakimbizi kujihisi kama wavamizi, lakini licha ya teknolojia hizi kupendekezewa serikali, hatujaona zikitekelezwa.
Katika mageuzi ya teknolojia, suala hili la ukosefu wa usawa wa kijinsia, kiumri, kieneo na kidini limejitokeza mno, na Afrika yafaa kuwa mstari wa mbele kuliondoa, kwani inafaidika zaidi na teknolojia hizi kuliko bara lingine lile.
Wakati wa kutumia teknolojia kuziba pengo la usawa katika masuala yote ya kimaisha ni sasa. Tukome kusubiri mafunzo kutoka mataifa ya nje.
Kilicho kwa sasa ni wasimamizi wa kambi hizi kuwasaidia maafisa wa GSMA na Vodafone kutekeleza wajibu wao wa kuwapa matumaini watoto wasiojua baba wala mama baada ya mataifa yao ya kiasili kukumbwa na vita na ghasia.