NGILA: Vijana wakome kufanyia mzaha janga la virusi hatari
Na FAUSTINE NGILA
INASIKITISHA mno kuwaona vijana wakiendelea kupuuza maagizo ya serikali yanayonuia kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.
Baadhi ya vijana niliosema nao kwenye mitandao ya kijamii wamedai eti serikali inawalazimisha kununua maski.
Wanasema hii ni mbinu ya wafanyabishara na serikali kuwapunja wananchi na kwamba hawana haja ya kununua maski. Mapuuza ya kipekee hayo.
Hawajui kwamba wanaambiwa wanunue kifaa hicho kwa manufaa yao wenyewe, kwa afya zao wenyewe.
Baadhi ya wanaofanya biashara ya teksi pia wamelalamika kuwa serikali inawazimia riziki kwa kuwataka kubeba abiria mmoja pekee badala ya wanne. Wanataka kila kiti kwa gari dogo kiwe na mteja!
Hivi najiuliza, upuuzi huu miongoni mwa vijana wakati vifo kutokana na virusi vya corona vimezidi 120,000 dunia, unatoka wapi?
Kuna wale wanaojishasha kuwa wao wana nguvu za kutosha mwilini na kuwa ugonjwa huo unawaua watu wazee.
Wengine wanasema virusi hivyo ni vya wale waliotangamana na watu waliosafiri mataifa ya nje.
Nawashangaa hawaelewi kati ya visa tulivyo navyo humu nchini, vingi ni maambukizi miongoni mwa watu ambao hawana historia ya kusafiri ng’ambo.
Kisha kuna wale vijana ambao wakitengwa kwa lazima wanageuza maeneo hayo kuwa ya burudani, ambapo wananunua pombe na kuandaa ngoma na densi kiholela huku wakipigana mabusu bila kujali.
Yaani ujinga wa kiwango hicho unawaingia vijana waliosoma, na kujihatarisha bila kukumbuka kuwa taifa la Amerika, kwa mfano, watu 1,800 hufariki kila siku.
Wengine nao wanapenda kukimbizana na polisi ili waonekane mabingwa wa mtaa, kwa kukaidi kutii kanuni za kafyu huku wenzao wakitumia njia za msituni kusafiri mashambani.
Ni kizazi ambacho hakiwezi kutulia, licha ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kukiomba kisaidie kupunguza kueneza virusi hivi.
Umri wa wastani nchini Kenya ni miaka 19, lakini hiyo haimaanishi kuwa walio na umri huo hawawezi kufariki kutokana na virusi vya corona.
Inakera sana kuwa vijana mpaka sasa hawajasikia anachokariri Bw Kagwe kila anapotoa takwimu mpya kuhusu ugonjwa huo.
Labda adhabu iliyowekwa ya faini ya Sh20,000 na kifungo cha miezi sita kwa wanaopatikana katika maeneo ya umma bila maski haitoshi na yafaa kuongezwa.
Tusiwe mabaradhuli wasiosoma chochote kutokana na mataifa yalioathirika zaidi kama Amerika, Italia, Uhispania na Ufaransa.
Ole wenu vijana msiosikia la mwadhini wala la mteka maji msikitini! Usimlaumu yeyote ukijipata taabani.