Makala

OBARA: Masaibu haya yatamfaa Ruto katika safari ya Ikulu 2022

November 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

KWA miezi kadhaa sasa, Naibu Rais William Ruto amejikuta kwenye kona mbaya huku akiwekewa visiki vya kila aina anapojikakamua kujiandaa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ifikapo uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Masaibu ya Bw Ruto yalianza kudhihirika wakati Rais Kenyatta alipotangaza vita vikali dhidi ya ufisadi.

Wandani wake walidai kwamba vita hivyo vililenga kulemaza uwezo wa naibu rais kuwa mwenyeji wa Ikulu uchaguzi wa urais utakapofanywa, huku wakilalamika vililenga watu wanaoweza kumsaidia kuafikia maazimio yake.

Punde baadaye, Rais Kenyatta alitangaza ushirikiano wake na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga.

Hatua hii pia ilionekana na wandani wa Bw Ruto kama mbinu ya Ikulu kumpendelea zaidi Bw Odinga kurithi urais ilhali, kulingana nao, kulikuwa na maelewano katika Chama cha Jubilee kwamba Rais Kenyatta atamuunga mkono naibu wake baada ya kukamilisha hatamu zake mbili za uongozi.

Makombora mengine ambayo yameelekezwa kwa naibu rais ni kuhusu ufufuzi wa kesi za ghasia zilizotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007 kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ubomoaji wa majengo ya kifahari ambapo hoteli zinazohusishwa na Bw Ruto zinalengwa, na sakata ya malipo kwa wakulima wa mahindi.

Mbali na haya, serikali inataka kusitisha kukodishia polisi nyumba ilhali inasemekana naibu rais ni miongoni mwa wamiliki wa nyumba hizo, na pia imesitisha ujenzi wa miradi mipya wakati ambapo Bw Ruto anazuru pembe tofauti za nchi kuzindua miradi na kujiongezea umaarufu kisiasa.

Kujikuza

Ingawa wandani wake wanalalamika kuhusu haya yote, naibu rais ni mwanasiasa ambaye amepalilia na kukuza umahiri wake wa kisiasa kutokana na visiki na makombora aliyokuwa akirushiwa tangu zamani.

Wakati alipokuwa chini ya mbawa za Rais Mstaafu Daniel arap Moi, wengi hawakumfahamu Bw Ruto kitaifa kwani alikuwa ‘mtu wa mkono’.

Baadaye, ilisemekana Rais Moi hakupendelea Bw Ruto awe mrithi wake kama kigogo wa kisiasa Rift Valley kwa sababu hakutoka katika kizazi cha kisiasa.

Inaaminika kuwa msukosuko huu ulimpa ari ya kujikuza kisiasa, akajiunga na Bw Odinga katika Chama cha ODM ambapo alifanikiwa kujizolea umaarufu mkubwa Rift Valley.

Katika ODM, naibu rais alipitia mengi, ikiwemo kusimamishwa kazi ya Uwaziri wa Kilimo kutokana na sakata ya mahindi iliyotokea mwaka wa 2010.

Unapotazama kwa makini, hali inayomkumba Bw Ruto hivi sasa si tofauti na masaibu ambayo yalimkumba awali yakampa umaarufu mkubwa wa kisiasa hadi akawa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya kwa hatamu mbili mfululizo.

Kuanzia kwa jinsi anavyodhalilishwa na familia ya Moi, madai ya kuwepo watu wanaomhangaisha katika chama chake cha Jubilee, kesi za ICC na sakata ya mahindi; haya ni masaibu ambayo amewahi kupitia awali.

Kinachosubiriwa kuonekana sasa ni iwapo Bw Ruto ataibuka mshindi jinsi alivyofanikiwa katika miaka ya awali.