Makala

OBARA: Mzozo wa maji Murang'a ni ithibati ya viongozi wazembe

October 15th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

KWA miezi michache sasa tumeshuhudia malalamishi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Kaunti ya Murang’a kuhusu usambazaji wa maji safi kwa wakazi wa kaunti hiyo.

Katika mstari wa mbele kuongoza malalamishi hayo ni Gavana Mwangi Wa Iria ambaye anataka Kaunti ya Nairobi iwe ikilipa ada kwa kaunti yake kutokana na kuwa maji mengi yanayotumiwa katika jiji hili kuu hutoka katika bwawa la Ndakaini linalopatikana Murang’a.

Kile ambacho gavana huyu anafanya ni uchochezi ambao haufai kuvumiliwa kwani naamini anaelewa vyema kuhusu sheria zinazosimamia mali asili nchini.

Kwa mtazamo wangu, ni aibu gavana huyu kujitokeza peupe na kutangazia taifa zima jinsi wakazi wa eneo lake wanavyotatizika kupata maji safi.

Huyu ni kiongozi ambaye anatumikia hatamu yake ya pili ya ugavana ilhali ana ujasiri wa kusimama mbele ya vyombo vya habari kutuambia kwamba katika muda wote ambapo amekuwa mamlakani, hakuna hatua aliyochukua kuondolea Wanamurang’a masaibu wanayopitia kuhusu uhaba wa maji safi.

Usambazaji wa maji kwa umma ni mojawapo ya majukumu ambayo serikali za kaunti zilirithi kutoka kwa mabaraza ya miji yaliyokuwepo kabla ya ugatuzi kuanza kutekelezwa mwaka wa 2013.

Sawa na majukumu mengine yaliyokuwa mikononi mwa mabaraza ya miji, usambazaji wa maji ulikumbwa na changamoto tele katika miji mingi wakati huo.

Hii ni kutokana na sababu mbalimbali, kuu ikiwa ni usimamizi mbaya na ubadhirifu wa fedha zilizopaswa kutumiwa kutumikia umma.

 

Awamu mpya

Wakati magavana walipoanza kuongoza, tumaini la wananchi wengi lilikuwa kwamba wangesuluhisha changamoto hizo. Katika sekta ya maji, ilitarajiwa wangeweka usimamizi bora na kujenga miundomsingi ya kisasa ili kuboresha huduma za kusambaza maji.

Kuna kaunti ambapo viongozi hawakupoteza muda walipoingia mamlakani kwani waliweka mikakati mara moja kusuluhisha tatizo hilo lakini inavyoonekana, Murang’a si miongoni mwazo.

Badala ya kuchochea wakazi wa kaunti yake dhidi ya Kaunti ya Nairobi, Gavana Wa Iria anastahili kuwajibika na awaeleze wakazi wake ukweli kuhusu anachotaka kutoka kwa jiji la Nairobi.

Ikiwa ni kweli kuwa anapigania haki yao kupata maji safi, kwa nini hadi sasa serikali yake haijawahi kuimarisha miundomsingi ya huduma hiyo muhimu?

Wakazi wa Murang’a wasikubali kuhadaiwa na tetesi za kiongozi wao ambazo nyingi hazina msingi.

Ni fedheha sana kwa gavana wa kaunti moja kutaka watu waliompigia kura, si mara moja bali mara mbili, waende wakalaumu gavana wa kaunti nyingine kwa ukosefu wa maji nyumbani kwao.

Kama malalamishi yake kwamba Nairobi inatumia maji ya Murang’a kwa njia isiyo ya haki, hili ni suala ambalo lingeanza kutatuliwa zamani na sasa wananchi wenzetu wa kaunti hiyo wangekuwa na afueni.

Isitoshe, kuna mbinu nyingine za busara za kutatua tatizo hilo ikiwa anayoyasema yana msingi badala ya kutumia uchochezi unaoweza kuathiri shughuli za jiji kuu la Kenya linalotegemewa zaidi kimataifa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na ya Kati.