OBARA: Wanakibra wawe makini katika uchaguzi mdogo
Na VALENTINE OBARA
KIVUMBI kimeanza kutifuka katika eneobunge la Kibra kwa maandalizi ya uchaguzi mdogo ambao umetokana na kifo cha aliyekuwa mbunge, marehemu Ken Okoth.
Kinachoonekana kwa sasa ni nafasi ya mahasimu wakuu wawili wa kisiasa nchini kupimana nguvu.
Kwa upande mmoja, kuna Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga na upande wa pili ni Naibu Rais William Ruto wa Chama cha Jubilee.
Katikati ya kimbunga kinachotarajiwa baada ya mchujo wa vyama na hatimaye kampeni zitakapoanza, kuna wakazi wa eneobunge hilo ambalo sehemu yake kubwa ni mtaa wa mabanda.
Kutokana na ushindani unaotarajiwa kati ya Bw Odinga na Bw Ruto, kuna hatari ya wapigakura kupotoshwa na kuishia kuchagua kiongozi asiyefaa.
Wakazi wa Kibra wametatizika kwa miaka mingi kwa kukosa huduma bora za kimsingi ikiwemo afya, usafi, elimu na makao bora.
Juhudi mbalimbali za kubadilisha hali hii katika miaka iliyopita ziligonga mwamba kwa sababu za kisiasa na vilevile ulafi wa kibiashara wa watu wachache wanaonufaika na umaskini wa wenzao.
Marehemu Okoth alifanya mengi kwa dhamira ya kuinua maisha ya Wanakibra lakini kwa bahati mbaya, akatuacha kabla ya kukamilisha mipango mingine aliyokuwa nayo.
Nilipotazama kwenye runinga hivi majuzi, niliona Chama cha ODM kupitia kwa kiongozi wake, Bw Odinga kikisema atakayepeperusha bendera ya chama hicho anafaa kuwa mtu aliye mwaminifu kwa chama hicho.
Ninafahamu fika kwamba kila chama hutaka wale watakaochaguliwa kupitia kwake wawe waaminifu.
Sina haja kueleza mengi kuhusu umuhimu huu kwa chama kwani tumeshuhudia jinsi uasi wa viongozi katika vyama vilivyowaingiza mamlakani unavyoibua misukosuko na kuathiri vibaya mwelekeo wa chama.
Licha ya haya, tumefika katika enzi ambapo uaminifu wa chama pekee haufai kutumiwa kama kigezo cha kumpokeza mtu tikiti ya kuwania uongozi wa kisiasa.
Inahitajika wakuu wa vyama vyote wazingatie umuhimu wa kuwezesha wananchi kuchagua viongozi wenye maono ya kimaendeleo ambayo yataboresha hali yao ya maisha.
Hata kama mgombeaji anachaguliwa kupitia kura ya mchujo, si siri kwamba wakati mwingi wakuu wa vyama huwa na usemi mkubwa kuhusu anayestahili kuchaguliwa na wajumbe.
Kama wakuu wa vyama wanaona vigumu kupigia debe wagombeaji kwa msingi wa uwezo wao wa kuleta maendeleo, basi wito wangu ni kwa wapigakura kujijali wao wenyewe.
Wachague kiongozi anayeweza kuwabadilishia hali ya maisha hata kama ni mgombeaji huru au anayetumia chama kidogo kisicho maarufu.
Chama kisiwe kiini cha kumchagua mtu atakayegeuka kuwa nduli kwa wapigakura pindi aingiapo enzini.