ONYANGO: Visa vya polisi kujiua vichunguzwe kwa kina
Na LEONARD ONYANGO
TUNAPOFUNGA mwaka, maafisa wa polisi ni miongoni mwa watumishi wa serikali ambao watakumbuka 2018 kwani walibadilishiwa sare na kupewa za rangi ya samawati.
Maafisa wa polisi watakumbuka mwaka huu kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta kuagiza walipwe marupurupu ya kuwawezesha kutafuta nyumba na kuishi popote wanapotaka mbali na vituo vyao vya kazi.
Hata hivyo, 2018 ni miongoni mwa miaka yenye huzuni kwa maafisa wa polisi.
Mwaka huu ulisheheni visa tele vya maafisa hao wa usalama kuua watu wa familia zao na kisha kujiua kwa kujifyatulia risasi. Mathalani, mwezi uliopita konstabo Cornelius Kipngetich, 28, aliyekuwa akihudumu katika Kituo cha Piave, Njoro alimuua mkewe Eunice Wambui kisha akajitoa uhai kwa kujipiga risasi.
Afisa wa kikosi cha GSU Anthony Lemayan Lenkisol ambaye pia alikuwa miongoni mwa madereva wa Inspekta Jenerali Joseph Boinnet, alijiua kwa risasi alipokuwa likizoni katika eneo la Mwamba, Narok mjini.
Mnamo Aprili Tirus Omondi, afisa wa polisi aliyekuwa akihudumu katika eneo la Takama, Kaunti ya Mandera alijinyonga nyumbani kwake huko Manyatta, Kisumu kutokana na madai kwamba alilemewa na madeni na hata kunyanyaswa kazini.
Kulingana na ripoti, mwendazake alionekana mwenye mzongo wa mawazo kabla ya kujiua.
Mnamo Oktoba, afisa wa Polisi wa Utawala (AP) wa umri wa miaka 35 alijiua kwa risasi mbele ya wenzake katika eneo laKandutura, Laikipia.
Inadaiwa kuwa afisa huyo wa polisi alikuwa akisumbuliwa na madeni na mizozo ya kifamilia.
Wiki iliyopita, konstabo Boaz Rotich Kipkosgei alijifyatulia risasi shingoni na kufariki papo hapo nje ya kanisa la Faza Fellowship, Kaunti ya Lamu, katika hali ya kutatanisha.
Mnamo Novemba, Konstabo Peter Wambiro Kagunda alijiua kutokana na sababu zisizojulikana katika Kaunti ya Bomet.
Mwezi huo huo, afisa wa polisi Peter Mawira alijitoa uhai katika kaunti ya Kitui kutokana na sababu zisizojulikana.
Hali ya huzuni ilitanda katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet baada ya maiti ya konstabo Michael Kipkoskei aliyekuwa akihudumu katika kituo cha Lokitaung kupatikana ikining’inia nyumbani kwake.
Hao ni baadhi tu ya maafisa wa polisi waliojitoa uhai mwaka huu.
Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba Idara ya Polisi haijachukua hatua kuchunguza kiini cha maafisa hao wanaojitoa uhai kiholela.
Idara ya polisi inafaa kuchukulia suala hilo kwa uzito.
Kwa mfano, ikiwa polisi anajiua kwa kunyanyaswa kazini, nani anawatesa? Idara ya polisi pia inafaa kufahamu sababu ya maafisa wake kujitosa katika madeni kupindukia kiasi cha kujiua.
Idarai hii haina budi kuchunguza kiini cha mizozo ya kifamilia miongoni mwa maafisa wa polisi na kuwawezesha kupata huduma za ushauri nasaha. Polisi ni binadamu sawa na wengine na wanastahili kusaidiwa.