Polisi na chifu wajificha kwenye shamba la ndizi kuepuka ghadhabu za wakazi
MAMIA ya wakazi wa kijiji cha Karungé eneobunge la Mathioya, Kaunti ya Murangá Jumapili walivamia kituo cha polisi na afisi ya chifu kisha kuwafurusha polisi waliokuwa wamejihami vikali.
Wakazi hao walisema walipata fununu kuwa mshukiwa sugu wa mauaji alikuwa akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Karungé na walitaka kumuua papo hapo wakisema hawakuwa na imani na mchakato wa kisheria.
Wakati wa uvamizi huo polisi na chifu walitoroka kisha wakajificha kwenye shamba la ndizi huku wakazi nao wakirusha mawe polisi wengine walipofika na kuwazidi nguvu.
Wakati wa makabiliano hayo, ilibidi polisi watumie vitoza machozi na kufyatua risasi hewani wakitaka wahakikishiwe usalama katika kijiji chao.
“Tunataka kumtendea mshukiwa huyo haki kwa sababu polisi nao hawaaminiki. Wamekuwa wakishirikiana na kuwalinda wahalifu hao,”akasema mmoja wa vijana wenye hasira wakati wa uvamizi huo.
Vijana hao walivamia seli na wakaondoka baada ya kugundua kuwa mshukiwa waliyekuwa wakimsaka hakuwepo. Waliapa kuwa hawatachoka hadi wamnase mshukiwa huyo na adabu pekee watakayomtia ni kumuua papo hapo.
Mnamo Agosti 4 mkazi Jamleck Irungu ambaye anafahamika sana alivamiwa akielekea nyumbani baada ya kutoka kujiburidisha kwenye baa.
Ripoti ya polisi ilisema kuwa Bw Irungu ambaye pia anafahamika kama Jamu wa Mbau alikuwa amegombana na mshukiwa huyo kwenye baa hiyo. Bw Irungu ambaye anauza mbao aliondoka kwenye baa hiyo saa mbili usiku baada ya kuzima kiu chake cha pombe.
Hata hivyo, alivamiwa akienda nyumbani kwake na kupigwa vibaya kisha akatupwa kwenye shimo la kina kifupi. Polisi wanashuku kuwa mshukiwa ambaye aligombana naye wakiwa kwa baa alihusika na kipigo hicho.
Bw Irungu alikimbizwa hadi Hospitali ya Murangá Level Five ambapo Dkt Leonard Gikera alisema alikuwa na majeraha mabaya ya kichwa.
Wakazi walilalamika kuhusu kutokamatwa kwa yeyote kuhusiana na kisa hicho na visa vingine ambavyo vimeripotiwa kijijini humo hapo awali.
Mkuu wa Polisi wa Mathioya Peter Karobia alisema kuwa bado wanaendeleza uchunguzi kuhusu kujeruhiwa kwa Bw Irungu na akawataka wakazi wawe watulivu.
“Tumewatuma polisi wengine warejeshe utulivu. Tutashughulikia malalamishi ya wakazi na kuwahakikishia usalama wao,” akasema Bw Karobia.
Hata hivyo, mkuu huyo wa polisi aliwataka wakazi wasichukue sheria mikononi mwao tena na kuvamia afisi ya chifu pamoja na kituo cha polisi.
Imetafsiriwa na Cecil Odongo