Makala

Punda wataisha uchinjaji haramu na wizi ukiendelea

Na KNA September 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KUNA haja ya kulinda punda ili wasitokomee ikizingatiwa ripoti za wataalamu kuwa idadi ya punda inazidi kupungua kila kuchao.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Utafiti wa Mimea na Mifugo nchini (Kalro), punda wamepungua sana na iwapo mikakati haitawekwa kuwalinda, hali itakuwa mbaya sana.

Hali hii imechangiwa na uuzaji wa punda kwa nia ya kuchinjwa pamoja na kukithiri kwa wizi.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa punda huwa na kiwango cha chini cha kuzaana kwa sababu ya muda mrefu wa kubeba mimba (miezi 12), uwezekano mdogo wa kuzaa hasaa kwa punda ambao hufanya kazi nyingi, mfumo wa kuwaweka katika mazizi nyumbani na muda mrefu wa kulea watoto wa punda.

Vile vile, punda wako katika hatari ya kufa kutokana na magonjwa kama vile pepopunda, kuharisha na pia matukio ya ajali.

Kupungua kwa asilimia 50

Ripoti ya Kalro ya 2022 inaonyesha idadi ya punda imepungua kwa takriban asilimia 50 kutokana na wizi na wakulima kukosa uwezo wa kununua punda wengine.

Uhitaji mkubwa wa nyama na ngozi ya punda katika soko la kimataifa ulisababisha kuanzishwa kwa vichinjio vya punda mnamo mwaka wa 2016.

Lakini baadaye vilifungwa mwaka wa 2020 baada ya visa vya wizi wa punda kukithiri.

Vichinjio vilivyopata kibali kuchinja punda vilikuwa Goldox Kenya Limited Mogotio, Star Brilliant, Naivasha, Silzah Limited, Lodwar na Fuhai Limited, Machakos.

Hazi za wanyama

Shirika la kutetea haki za wanyama la Farming System Kenya (FSK) limesikitishwa na kinachoendelea katika jumuiya ya mifugo wa uchukuzi.

Afisa wa Programu za FSK Samuel Chege anasema kama vichinjio hivyo havikufungwa, idadi ya punda ingeshuka kutoka 1.9 milioni mwaka wa 2016 hadi chini ya 500,000 mwaka wa 2022.

Hata hivyo, aliibua wasiwasi kuhusu visa vya uchinjaji punda katika misitu.

“Tuna ushahidi punda wanachinjwa msituni Ewaso Kedong, Kaunti ya Kajiado. Hii ni kinyume cha marufuku iliyotolewa na serikali,” alisema.

 Bw Chege anasema visa hivi vimeongeza bei ya punda lakini wakulima wengi hawako tayari kuwauza kwa sababu ya umuhimu wao.

“Wakulima wanajizatiti kulinda wanyama dhidi ya wizi kwa kuunda mazizi yanayofungwa hasaa usiku,” alisema.

Jamii za matabaka ya chini zinazotegemea punda kutega uchumi hupata kati ya Sh1000 na Sh1500 kwa siku.

“Wanawake wengi huchukulia punda kama wake-wenza kwa sababu wanawasaidia kuteka maji, kubeba mazao ya shambani, kutega uchumi na kuwa njia ya usafiri,” alisema, akieleza kuwa katika baadhi ya maeneo, maziwa ya ng’ombe huwa matamu na hupewa watoto na wagonjwa.

Utashi wa nyama ya punda

Uhitaji wa nyama na ngozi ya punda katika mataifa kama vile China umekuwa hatari kwa punda.

“Ngozi ya punda hutumiwa kuunda dawa ya kienyeji iitwayo ejiao. Ejiao huundwa kwa kutumia kiungo kinachominywa kutoka kwa ngozi ya punda iliyochemshwa. Inasemekana kuwa, dawa hii huongeza damu, kuchelewesha kuzeeka, kuongeza nguvu za kiume, kutibu athari ya dawa za kansa, kuzuia hali ya kutozaa, kuharibika kwa mimba na mabadiliko ya utaratibu wa hedhi,” alisema Bw Chege.

Dkt Yegon Kibet wa shirika la FSK ameomba washikadau kushirikiana ili kulinda punda akiomba wananchi kutoa habari wakiona punda wengi wakisafirishwa.

Alisema uchinjaji wa punda msituni ni hatari kwa wakazi  sababu wanaweza kupata magonjwa kama vile kimeta.

Dkt Yegon anawarai wakulima wahakikishe punda wao wanatibiwa.

Hivi maajuzi, punda 68 walitwaliwa walipopatikana katika soko la Mulot wakisafirishwa kuelekea Mji wa Narok.

Wakati huo, wasafirishaji walitiwa mbaroni walipokutwa hawana leseni ya uchukuzi wa punda.

Punda hao walipelekwa katika shirika la haki na utunzaji wanyama la Kenya Society for the Care and Protection of Animals Naivasha.

Wachukuzi walikamatwa na kushtakiwa kortini kwa kusafirisha punda bila leseni.

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan