Raila alakiwa kishujaa, wafuasi wakiteka shughuli jijini na JKIA
UMATI mkubwa ambao unaendelea kusindikiza mwili wa Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga nyumbani, ulisababisha ratiba ambayo iliwekwa na serikali ibadilishwe.
Bw Odinga ambaye mwili wake ulifika nchini sasa atapelekwa uwanja wa Moi Kasarani ambako wafuasi wake na Wakenya watatazama mwili wake.
Taarifa zilizotumwa na serikali zilisema kuwa mwili wa Raila sasa utapelekwa katika makafani ya Lee kisha upelekwe Kasarani.
Hata hivyo, kufikia wakati wa kuchapisha taarifa hizi bado msafara wa mwili wa Bw Odinga upo kwenye barabara ya Mombasa.
Mwili wa Raila ulipokelewa kishujaa na waombolezaji ambao walisitisha shughuli katika uwanja wa ndege wa JKIA, baadhi wakiingia ndani ya ndege iliyobeba mwili wa Raila.
Licha ya usalama mkali, baadhi waliwazidi wanajeshi na kufikia jeneza ambalo lilikuwa limebeba mwili wa Raila huku wakiomboleza bila kikomo
“Ni babake pekee ndiye anaweza kutuliiza. Aamke atutulize,” wakasikika baadhi ya waombolezaji wakisema. Wengi walizidiwa na hisia huku wakimkaribisha kiongozi wanayempenda mara hii akiwa kwenye jeneza.
Rais William Ruto, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, familia ya marehemu Raila, viongozi wa serikali na wanasiasa ambao walikuwa wamefika kuupokea mwili kwa njia rasmi hawakupata nafasi kwa sababu ya umati ambao ulikwepo na ilikuwa wazi ratiba haingeendelea.
Msafara wa Rais Ruto na viongozi wengine ulisalia JKIA kisha baadaye ukafuata ule ambao umebeba mwili wa Bw Odinga ambao bado upo njiani kuelekea Lee.
Baadhi ya wafuasi wa Bw Odinga, wameapa kuwa lazima wao ndio waongoze na kuelekeza ratiba ya kuagwa kwake. Katikati mwa jiji la Nairobi, kila aliyetembea jijini alibeba matawi kama ishara ya kuomboleza huku pikipiki na magari yakipiga honi.
Haya yanafanyika huku wakazi wa Kisumu nao wakisubiri kwa hamu na hamumu kupokea mwili wa shujaa huyo ambaye amekuwa na nyapara
Raila atazikwa Jumapili hii, mazishi ambayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wengi ndani na nje ya nchi.