Raila avuna matunda ya handisheki na Ruto
MKATABA wa ushirikiano ambao Kiongozi wa ODM Raila Odinga alitia saini na serikali ya Kenya Kwanza unaendelea kuzaa matunda huku washirika wake wakinufaika na nyadhifa za makatibu wa wizara.
Katika mabadiliko ambayo Rais William Ruto alifanyia makatibu wa wizara Alhamisi, Machi 20, 2025, washirika wa Bw Odinga waliteuliwa kuhudumu katika Idara za wizara muhimu.
Katika mabadiliko hayo, Rais Ruto aliteua makatibu 14 wapya, zaidi ya 10 wakiwa washirika wa Bw Odinga na kuwahamisha sita kupisha wale wa waziri mkuu huyo wa zamani.
Katika taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Ikulu, Hussein Mohammed, rais alimhamisha Amos Gathecha kutoka wizara ya utumishi wa umma na kumteua kuwa Naibu Mkuu wa Huduma za Umma.
Prof Edwin Kisiangani, ambaye alikuwa akihudumu katika Wizara ya ICT, sasa atahudumu kama mshauri na mwanachama wa baraza la washauri wa kiuchumi wa rais.
Makatibu wapya 14 wanaohusishwa na Raila ni pamoja na Dkt Jane Kare Imbunya (Idara ya Utumishi wa Umma), Bi Regina Akoth Ombam (Idara ya Biashara), Cyrell Wagunda Odede (Idara ya Uwekezaji wa Umma katika Hazina ya Kitaifa na Mipango ya Uchumi.
Dkt Caroline Wanjiru Karugu ambaye alikuwa mwanachama wa kampeni ya Raila katika uchaguzi mkuu wa 2022 na ule wa uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) Idara ya Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) naye Dkt Oluga Fredrick Ouma akisimamia Idara ya Huduma za Matibabu, Wizara ya Afya.
Bi Judith Pareno ambaye aliwahi kusimamia bodi ya uchaguzi ya ODM na Mshirika mwingine wa Bw Odinga atasimamia Haki za Binadamu na Masuala ya Katiba katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Idara ya Haki huku Carren Ageng’o Achieng akisimamia Idara ya Huduma za Ustawi wa Watoto katika Wizara ya Kazi na Ulinzi wa Jamii.
Bw Ahmed Abdisalan Ibrahim aliteuliwa kuwa Katibu wa Idara ya Uratibu wa Serikali ya Kitaifa katika Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri.
Dkt Bonface Makokha atakuwa Katibu wa Idara ya Mipango ya Uchumi katika Hazina ya Kitaifa na Mipango ya Uchumi naye Prof Abdulrazak Shaukat atasimamia Idara ya Sayansi, Utafiti na Ubunifu, Wizara ya Elimu katika wadhifa huo huo.
Rais William Ruto pia alimteua Bw Stephen Isaboke kuwa Katibu, Idara ya Utangazaji na Mawasiliano ya Simu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidijitali kuchukua nafasi ya Profesa Edward Kisiang’ani ambaye ameteuliwa mshauri na mwanachama wa baraza la kiuchumi la rais.
Bw Michael Lenasalon aliteuliwa katibu Idara ya Ugatuzi, Afisi ya Naibu Rais kuchukua nafasi ya Terry Mbaika ambaye alihamishiwa Idara ya Maendeleo ya Anga na Usafiri wa Angani, Wizara ya Barabara na Uchukuzi.
Bw Fikirini Katoi Kahindi Jacobs atakuwa Katibu, Idara ya Masuala ya Vijana, Wizara ya Masuala ya Vijana na Michezo huku Bw Aden Abdi Millah akiwa Katibu, Idara ya Uchukuzi wa Baharini na Masuala ya Majini, Wizara ya Madini, Uchumi wa Majini na Masuala ya Baharini.
Aliyekuwa katibu wa uhamiaji Prof Julius Bitok alihamishwa kutoka Idara hiyo hadi Idara ya Elimu ya Msingi, Wizara ya Elimu akibadilishana na Dkt Belio Kipsang.
Bw Ismael Madey naye alihamishwa kutoka Idara ya Masuala ya Vijana na Uchumi wa Ubunifu hadi Idara ya mipango Maalum, Wizara ya Utumishi wa Umma.
Aliyekuwa katibu wa Huduma za Matibabu katika wizara ya afya Harry Kimtai alihamishwa hadi Idara ya Madini, Wizara ya Madini. Kimtai alimpisha Dkt Oluga, mshirika wa Bw Odinga.
Aliyekuwa Waziri wa Afya, Susan Nakhumicha, alirudi katika serikali, miezi tisa baada ya kupoteza wadhifa wake wakati huu akiwa Balozi wa Kenya katika Shirika la Makao la Umoja wa Mataifa(UN-Habitat) jijini Nairobi.
Mbali na Nakhumicha, Rais pia aliwateua James Buyekane Muhati na Abdi Dubat Fidhow kuwa mabalozi wa Kenya katika Guangzhou, China, na Arusha, Tanzania, mtawalia.
Bw Peter Tum aliteuliwa kuwa Balozi wa Kenya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku Alfred K’Ombundo akiteuliwa kuwa Naibu Mkuu wa Ubalozi wa Kenya nchini Ubelgiji.
Katika taarifa rasmi, Ikulu ilisema waliteuliwa kwa mujibu wa Kifungu cha 132 (2) (e) cha Katiba.
Kulingana na Hussein Mohamed, majina yao tayari yamewasilishwa kwa Bunge la Taifa kuthibitishwa inavyohitaji sheria.