BambikaMakala

Richarlson akosana na majirani kuhusu kero za mbwa wake

Na MWANDISHI WETU March 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

FOWADI wa Tottenham Hotspur, Richarlison Andrade, 27, anachunguzwa na Shirika la Kulinda Wanyama nchini Uingereza (RSPCA) kuhusu madai kuwa kelele za majibwa yake mawili ni kero kwa majirani.

Sogora huyo wa zamani wa Everton ametakiwa pia na majirani kuhama mtaa iwapo hatakoma kucheza muziki kwa sauti ya juu kila anapoandaa dhifa za usiku zinazohudhuriwa na marafiki wa karibu ambao hushiriki ulevi nyumbani kwake mara kwa mara usiku kucha.

Majirani wamelalamikia pia mazoea ya Richarlison kuelekeza mipira katika maboma yao kila anapojifanyia mazoezi katika uwanja mdogo wa mpira ulioko nyumbani kwake.

“Mipira hiyo huchafua bustani za maboma yetu, huangukia paa na huvunja vioo vya milango na madirisha,” akasema jirani mmoja aliyehojiwa na gazeti la The Sun.

Jirani mwingine mwenye umri wa miaka 77 alisema: “Karamu za usiku anazoziandaa hutunyima usingizi. Tumemripoti kwa RSPCA kwa sababu majibwa yake hubweka usiku bila kukoma. Hakuna raha kabisa ya kuishi hapa tangu Richarlison ahamie mtaa huu.”

“Hivi majuzi alikuwa na dhifa kubwa na akaalika bendi iliyocheza muziki usiku mzima. Sauti ilikuwa ya juu sana hadi kuta za nyumba zetu zikaanza kurindima na kutetemeka. Richarlison hatujali kabisa. Heri atuondokee,” akaongeza.

Richarlison anamiliki jibwa la rangi ya kijivu linaloitwa Acerola na jingine la rangi ya chokoleti katika kasri lake la Sh670 milioni, eneo la London Kaskazini.

Kwa mujibu wa majirani, majibwa hayo hutoroka katika boma la Richarlison mara kwa mara usiku na kuanza kubwekea kila mahali kwenye barabara ya A inayounganisha makazi yao na duka kubwa lililo karibu.

“Majibwa yana sauti kubwa za kutisha. Hukimbia kila mahali yakizunguka. Tunatumai RSPCA itampokonya majibwa hao nasi tumshinikize ahamie kwingineko,” akasema jirani mwingine.

Sogora huyo anayedumishwa kwa mshahara wa Sh24 milioni kwa wiki, aliwahi kutumia mtandao wa X kutuma ombi la kusaidiwa kutafuta mbwa wake, Acerola, aliyetoroka nyumbani na kukosa kurejea.

Jibwa hilo lilipatikana saa mbili baadaye ujumbe wa Richarlison uliposambazwa mitandaoni na takriban mashabiki 1,000.

Msemaji wa Spurs amesema klabu itawasiliana na sogora huyo pamoja na wawakilishi wake kuhusiana na malalamishi ya majirani ambao wamekerwa na vituko vya mvamizi huyo raia wa Brazil.