Makala

Ruto atoa onyo kwa Gen Z wanaopanga kuandamana Alhamisi

Na SAMMY WAWERU August 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HUKU vijana barobaro nchini wakipanga kuandamana kesho, Alhamisi, Agosti 8, 2024, Rais William Ruto ametoa onyo kali akisema hatakubali siasa za kurejesha Kenya nyuma.

Vijana hao wachanga, maarufu kama Gen Z, wameapa kuandaa maandamano ya kitaifa, katika kile wanahoji wanataka serikali kushusha gharama ya maisha na kushughulikia masuala yao.

Kiongozi wa nchi, Dkt Ruto, hata hivyo, amesema serikali yake haitaruhusu jukwaa la siasa za uharibifu nchini.

Hata ingawa hakuwataja kama wanavyojulikana, Gen Z, akihutubu Jumatano, Agosti 7 katika Kaunti ya Embu, Rais alisema hataitikia watu wapange fujo kupitia maandamano.

“Hatutaki siasa ya fujo, maafa, na kuharibu mali ya watu. Tunataka siasa ya kupanga vile Kenya itakuwa bora kuliko ilivyo sasa,” Rais Ruto akasema.

Alitoa onyo hilo akihutubu katika mkutano wa umma eneo la Kanyuambora, Mbeere Kaskazini ambapo amezuru Embu kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Gen Z wameapa kuandaa maandamano wanayosema yatakuwa wa kihistoria tangu wazindue oparesheni kukosoa serikali ya Kenya Kwanza.

Maarufu kama ‘Nane Nane’, vijana wanaendelea kuyavumisha kwenye majukwaa mbalimbali mitandaoni.

Akizungumza na wakazi wa Embu, Ruto aliwashirikisha kwa maswali akitaka kujua ikiwa wanayaunga mkono au la.

“Kenya ni nchi ya demokrasia, Kenya ni chi ya amani, Kenya ni nchi inayofuata Katiba na sheria. Ama watu wa Embu mnasemaje? Mnasema tuendelee na amani na maendeleo, ama mnataka watu watupangie fujo?” kiongozi wa nchi akauliza.

Umma uliskika ukimtaka Rais adumishe amani, majibu yanayofasiriwa kuwa kinaya na malalamishi hasa wanapoendeleza shughuli zao za kila siku kufuatia kuendelea kupanda kwa gharama ya maisha na uchumi.

“Tuendelee na amani? Mnataka amani ama mnataka watu watuletee fujo?” akazidi kuwadadisi.

“Mnataka amani? Wale wanakubaliana na mimi tuwe na nchi ya amani nione kwa mkono…” akaendelea Rais.

Aidha, waliohudhuria mkutano huo wa hadhara waliskika wakimshangilia kiongozi wa taifa huku wakiinua mikono kuitikia semi zake.

Kabla ya kutoa onyo kwa wana Gen Z, Rais Ruto alitoa mapochopocho ya ahadi za maendeleo kwa wakazi wa Embu.

Aliahidi kuwaboreshea barabara, kuunganisha stima kwa maboma yasiyo na nguvu za umeme, maji na ujenzi wa masoko.

Rais aliskika akihoji lengo lake ni kuona Kaunti ya Embu inasheheni pesa.

Gen Z wameonekana kukaidi amri ya Rais, minong’ono ikihoji wanataka mawaziri waliorejeshwa kazini kuondolewa mara moja.

Mapema Julai 2024, Ruto alivunja baraza lake la mawaziri kufuatia maandamano yaliyotikisa taifa na ulimwengu.

Vijana walikuwa wanashinikiza kutimuliwa kwa baadhi ya mawaziri.

Maafa, majeruhi na uharibifu wa mali ulishuhudiwa maeneo yaliyochacha maandamano.