Ruto na Gachagua ‘wanavyovuana’ nguo hadharani
RAIS William Ruto na aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua sasa wameamua kuharibiana sifa hadharani huku uhasama wao ukiendelea kutokota.
Kwenye mahojiano na wanahabari wa vituo vya habari kutoka Mlima Kenya Jumatatu jioni, Machi 31, 2025 Dkt Ruto alidai alimwokoa Bw Gachagua kwa kuteuliwa kama mgombea mwenza wake, katika uchaguzi mkuu wa 2022, licha ya kukataliwa na wabunge wa Mlima Kenya.
Aliongeza kuwa baada ya wao kushinda uchaguzi wa urais na kuingia mamlakani, mbunge huyo wa zamani wa Mathira aligeuka msumbufu akimlalamikia kila mara kwamba anahujumiwa na watu kadhaa serikalini.
Vile vile, Rais Ruto alidai kuwa wakati mmoja Bw Gachagua alimwitisha Sh10 bilioni, la sivyo amwangushe kisiasa katika uchaguzi mkuu wa 2027.
“Nilimteua kuwa mgombea mwenza wangu licha ya kwamba wabunge wa Mlima Kenya hawakuwa wakimtaka. Katika kura iliyopigwa katika makazi ya Naibu Rais huko Karen, Profesa Kindiki alipata kura 27 huku akipata kura tano pekee. Hata hivyo, niliamua mwenyewe kumpata nafasi hiyo kwa sababu ni mwenye umri mkubwa karibu na wangu,” akaeleza akiwa katika Ikulu ndogo ya Sagana.
Lakini, Dkt Ruto akaongeza, Gachagua alianzisha vita vikali na wabunge hao hao kutoka Mlima Kenya akiwashikiniza wamtambue kama msemaji wa eneo hilo kisiasa.
“Vile vile, alilalamika kuhusu wabunge hao kama vile Ndindi Nyoro na mbunge mwingine mwanamke. Alishinda akinilalamikia kila mara, akiwemo mwanablogu Itumbi, Farouk na wengine. Nilimwambia aachane vita hivyo vidogo na awafanyie wananchi kazi. Hapo ndipo aliitisha Sh10 bilioni la sivyo aniharibie nisichaguliwe tena. Nilikataa vitisho hivyo,” akaeleza.
Mbunge wa Mathira Eric Wamumbi pia amewahi kudai kuwa alimtaka Rais Ruto ampe kiasi hicho cha pesa kama “shukrani ya kumsaidia kupata uungwaji mkono kutoka Mlima Kenya katika uchaguzi mkuu uliopita.
Rais Ruto, pia, alieleza vile alivyozima majaribio mawili ya wabunge kumtimua Bw Gachagua huku akijitenga na hoja ambayo hatimaye ilipitishwa Oktoba 8, 2024 na jumla ya wabunge 381.
“Yeye ndiye alichochea kutimuliwa kwake ambako kulifanywa kwa mujibu wa Katiba na sikuwa na mamlaka kuzuia hatua hiyo,” akaeleza.
Dakika chache baadaye, Bw Gachagua alijibu madai ya Dkt Ruto akiyataja kama “yasiyo na mashiko” akimsuta kiongozi wa taifa kwa kudanganya na kupotosha wananchi.
“Sasa nashawishika uongo ni tatizo la kiakili. Tishio kubwa kwa nchi yetu ni kuwadanganya Wakenya bila kupepesa jicho, na kufeli kwa kiongozi kuwaelekeza watu wake kuweka pamoja uongo wao. Nalilia nchi yangu,” akasema kupitia akaunti yake ya mtandao wa X na pia Facebook.
Bw Gachagua, hata hivyo, hakukana madai ya Rais Ruto dhidi yake, moja baada ya nyingine.
Itakumbukwa kwamba siku mbili kabla ya Rais kutoa madai hayo, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah alidai kuwa mwaka jana mbunge huyo wa zamani wa Mathira alitaka afisi yake itengewe Sh250 milioni zaidi za matumizi ya kisiri.
“Alitaka Rais aamuru kwamba atengewe pesa hizo licha ya kwamba tayari afisi yake ilikuwa imegawiwa Sh750 milioni za matumizi kama hayo. Rais alipokataa, ndipo akaanza kumpiga vita na kupinga mipango ya serikali,” akaeleza Bw Ichung’wah ambaye ni mbunge wa Kikuyu, kwenye mahojiano katika mtandao wa “Kogi’s Corner”.
Januari 27, mwaka huu, Bw Gachagua alipuuzilia mbali mpango wa serikali wa Ujenzi wa Nyumba za Gharama Nafuu (AHP) akidai lengo lake kubwa sio kutoa nafasi za ajira bali ni kutajirisha wandani wa Rais Ruto.
“Awali, tuliamini kuwa mpango huo ulikuwa wa kubuni nafasi za ajira. Baadaye, ilinipambazukia kuwa hii ni njama ya Ruto kutajirisha marafiki zake wanaoendesha biashara ya kuuza vyuma, simiti, mabati na vifaa vingine. Hii ndio maana nilikataa kupigia debe mpango huo na akaanza kunichukia,” akasema jijini Nairobi wakati wa uzinduzi wa makao makuu mapya ya Democratic Action Party of Kenya (DAP-K).
Bw Gachagua aliyeandamana na wanasiasa wengine wa upinzani, pia, alidai kuwa ni kwa misingi hiyo hiyo ambapo alipinga mipango mingine ya serikali kama Bima mpya ya Afya ya Jamii (SHA) na mpango wa utoaji wa zabuni wa kampuni ya Adani kutekeleza miradi katika sekta ya kawi.
Hii ndio maana kwenye mahojiano yake na wanahabari Jumanne, Dkt Ruto alimsuta Bw Gachagua kwa kufeli kutetea ajenda za serikali alipohudumu kama naibu rais.
“Nilipohudumu kama Naibu Rais ningeenda katika kila runinga kuzitetea sera za serikali. Lakini kwa miaka miwili na nusu ambapo alihudumu kama naibu rais Gachagua alikataa kabisa kufanya hivyo. Ina maana kuwa hakujitolea kuuza ajenda yetu,” akaelaza.