Sababu za paka wa Kisiwani Lamu kunenepa
MARA nyingi unapopita kwenye mitaa, vishoroba na baraste ya mbele ya mji wa Kale wa Lamu, utagundua kuwa paka wengi eneo hilo ni wanene na wenye afya nzuri ya mwili kwa jumla.
Kinyume na maeneo mengine ya nchi ambapo utampata paka, hasa wale wa kuzurura mitaani, akiwa amekonda na mwenye mtazamo wa kuhurumisha, paka wa kisiwani Lamu kwa upande mwingine wamebarikiwa na mwili wa kuvutia na unene wa kiasi cha haja.
Taifa Dijitali ilizama chini kutaka kujua hasa ni nini kinachopelekea mnyama paka kisiwani Lamu kuwa na siha njema kila wakati.
Je, hawa ni ‘Paka Jini’ kama ilivyo dhana ya wengi kwamba ukienda mwambao wa Pwani ujue paka yeyote umuonaye mtaani ama kichochoroni sio paka?
Abubakar Kupi, mmoja wa wapenda paka mashuhuri mjini Lamu, alisema idadi kubwa ya wakazi kisiwani humo wamejitolea kwa hali na mali katika kuyatunza maisha ya paka bila kujali ni wake, wa jirani ama hata yule wa kuzurura mitaani.
Bw Kupi tayari anaonekana akiwa ameshikilia samaki mkubwa mkononi aliyemvua kutoka Bahari Hindi huku akizingirwa na makumi ya paka forodhani.
“Huyu samaki umuonaye nimevua nitamkatakata minofu midogomidogo kwa minajili ya kulisha hawa paka. Ni marafiki zangu hawa. Kila siku mimi huhakikisha maisha yao ni mazuri. Watakula huyu samaki freshi. Furaha yao ni furaha yangu,” akasema Bw Kupi.
Hata hivyo, anapinga vikali madai kwamba wengi wa wapenda paka huwa wanawatumia kama majini ya kuwaletea mali au utajiri.
Majini ni viumbe wanaosadikika kuishi katika mazingira ya kila aina. Baadhi ya watu wanaamini ni viumbe wenye uwezo mkubwa wa kufanya vitu tofautitofauti.
Majini wana uwezo wa kujibadilisha kuwa katika hali waipendayo. Aweza kuwa paka, mbwa, na hata nyoka.
Kwa Bw Kupi, yeye anashikilia kuwa si wote wanaopenda paka au paka umuonaye tayari ni jinni.
“Mimi hawa paka uonao ni kweli ni paka. Siyo majini hawa. Hiyo ni habari potovu na ya tangu jadi tu ambayo imekuwa ikienezwa, hasa na watu kutoka bara. Wanahusisha paka wanaopatikana maeneo ya Pwani na ushirikina, almaarufu ‘paka jini.’ Ila hawa wetu wa Lamu ni wa kikweli.

Bw Mohamed Swaleh, mmoja wa wapenda paka Lamu, anafafanua kuwa sababu kuu inayofanya paka wengi wa Lamu kunenepa ni kutokana na kula vyakula freshi moja kwa moja kutoka Bahari Hindi, hasa samaki.
Bw Swaleh anasema ni muhimu kwani ukila mwili wake unapata asilimia kubwa ya protini na fatty acids ambazo mwili huhitaji kwa wingi.
“Kinyume na paka wa sehemu zingine za Kenya ambao hupatiwa vyakula vilivyopitia mifumo mingi kutayarishwa na kuhifadhiwa kwa muda mrefu mikebeni kabla ya kutumiwa na wanyama kama paka, hawa paka wetu hapa wao hula samaki safi na motomoto kutoka baharini. Samaki wana mafuta ambayo huufanya mwili kunenepa haraka,” akasema Bw Swaleh.
Bi Nana Bakari alisema yeye binafsi hufika sokoni kila siku kununua kilo kadhaa za samaki wabichi na matumbo na kuwalisha paka wanaomtembelea kila asubuhi.
“Kuna paka zaidi ya 50 ambao kufikia saa kumi na moja unusu asubuhi huwa wamekusanyika mlangoni kwangu wakisubiri niwape chakula. Mimi huwalisha vyema licha ya kwamba si wangu na nasikia raha. Mambo yangu hunyooka tu,” akasema Bi Bakari.
Kiongozi wa dini ya Kiislamu kisiwani Lamu, Bw Abdulkadir Mau, aliwahmiza wakazi kupenda wanyama na kukidhi mahitaji yao.
Alisema kuwakirimu wanyama kama paka ni mojawapo ya ibada kwa Muislamu.
Alisema paka wengi Lamu wanatunzwa vizuri kutokana na watu kuthamini maelekezo ya dini yanayosisitiza kuwa pamoja na kuonyesha huruma kwa wanadamu wenzetu, Uislamu pia umewataka wawe na huruma kwa wanyama.
“Utapata wengi wakijikaza hapa kisiwani kuwatunza paka na viumbe wengine. Hivyo ndivyo Mola atakavyo. Ukiwa katili kwa wanyama ni dhambi inayoweza kukuingiza motoni,” akasema Bw Mau.
Alisisitiza umuhimu wa huruma kwa viumbe wote wenye uhai, akitaja mojawapo ya hadhithi za Mtume (S.A.W) kwamba mwanamke alitiwa motoni kwa sababu alimfunga paka bila kumlisha au kumwachia huru, ambapo angeweza kwenda huku na huku na kujilisha kutokana na wadudu na kadhalika.
Lamu ina zaidi ya paka 10,000 wanaopatikana kwenye visiwa mbalimbali vya eneo hilo.