• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
SAKATA YA  MAHINDI: Serikali ilivyopoteza mabilioni

SAKATA YA MAHINDI: Serikali ilivyopoteza mabilioni

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI ilipoteza mapato ya kima cha Sh16.7 bilioni wakati Hazina ya Kitaifa iliporuhusu uagizaji mahindi kutoka nje bila kulipiwa ushuru kati ya mwezi Mei na Oktoba 2017 hatua ambayo ilipelekea uagizaji wa bidhaa kupita kiasi.

Hasara hiyo ya mapato kutokana na ushuru huenda ikawa juu hata zaidi ikiwa pesa ambazo zingekusanywa kutokana uagizaji wa sukari na maziwa bila kulipiwa ushuru pia ingejumuishwa katika hesabu hiyo.

Waziri Msaidizi wa Fedha Nelson Gaichuhie Jumatano aliiambia kamati ya seneti inayochunguza sakata ya uagizaji mahindi kinyume cha sheria kwamba jumla ya yano 944,530 ya mahindi iliingizwa kutoka nje katika kipindi hicho kwa ajili ya kukabiliana na uhaba wa bidhaa hiyo nchini.

“Shehena moja ya mahindi meupe ilipaswa kutozwa ushuru wa Sh15.1 bilioni na tani 148,562 ya mahindi ya manjano ambayo ingepasa kulipiwa ushuru wa kima cha Sh1.6 bilioni,” Bw Gaichuhie akaambia kamati hiyo ambayo pia inachunguza chanzo cha mzozo unaoendelea katika sekta ya mahindi nchini wakati huu.

Alifika mbele yake Jumatano katika ukumbi wa County, Nairobi akimwakilisha Waziri wa Fedha ambaye hakufikwa kutokana na shughuli nyingi za kikazi zilizokuwa zimembana.

Bw Gaichuhie aliimbia kamati hiyo ya muda inayoongozwa na Seneta wa Uasin Gishu Margaret Kamar kwamba Wizara ya Fedha iliwaruhusu kampuni na watu binafsi kuingiza mahindi nchini bila kulipiwa ushuru kufuatia ombi iliyopokea kutoka kwa Wizara ya Kilimo.

Hata hiviyo, Waziri huyo msaidizi alishindwa kueleza ni kwa nini Wizara ya Kilimo ilitoa ombi hilo la uagizaji wa mahindi kutoka nje ilhali wakati huo Shirika la Kuhifadhi Nafaka kwa Matumizi ya Dharura (Strategic Grain Reserve-SGR) lilikuwa chini ya Wizara ya Ugatuzi.

Hata hivyo, Bw Gaichuhie alieleza kuwa amri ya uagizaji wa mahindi ilitolewa na Jopo Shirikishi lililobuniwa na Serikali kujadili hatua zinazofaa kuchukuliwa kukabiliana na uhaba wa mahindi nchini. Hali hiyo iliopelekea ongezeko la bei ya unga hadi kufikia Sh200 kwa paketi moja ya kilo mbili katika maduka kadhaa nchini.

“Hata hivyo, jopo hilo halikuweka kiwango cha mahindi ambacho kilipaswa kuagizwa kutoka nchini hali iliyopelekea mashirika na watu binafsi kuingiza mahindi nchini kupita kiasi hali iliyopelekea Wizara ya Fedha kukosa mapato,” akaambia kamati hiyo.

Hata hivyo Bw Gaichuhie alishindwa kueleza sababu iliyopelekea Wizara ya Fedha kutoa ilani nyingi kwenye gazeti rasmi la serikali iliyoongeza muda wa kuagizwa kwa mahindi kutoka Oktoba 1, 2017 hadi Oktoba 30, mwaka huo.

Bi Kamar na Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito walitaka kujua ni kwa nini wizara ya fedha ilitoa notisi ya kuongeza muda wa uagizaji mahindi nchini mwezi wa Oktoba wakati ambapo wakulima wahindi nchini walikuwa wameanza kuvuna zao hilo.

Bw Gaichuhie pia alishindwa kueleza ni kwamba Wizara ya Fedha ilifeli kudhibiti kiwango cha mahindi kilichopaswa kuagizwa ilivyofanya kuhusiana na uagizaji wa maziwa ya unga katika kipindi hicho (Mei hadi Oktoba 1, 2017).

“Tulitoa idhini hiyo kwa nia njema. Tulipopokea ombi kutoka kwa Wizara ya Kilimo hatukuwa na sababu yoyote ya kuibua shauku. Tuliamini kuwa maafisa wa wizara hiyo walifanya utathmini kuhusu upungufu wa mahindi kabla ya kuwasilisha ombi kwetu,” akasema.

Bw Mbito aliisuta Wizara ya Fedha kwa kufeli kuchambua ombi la Wizara ya Kilimo, akidai “ilitekeleza majukumu yake kama roboti.”

Baada ya serikali kutoa idhini hiyo, wafanyabiashara walinunua mahindi kutoka Mexico na Afrika Kusini na kuuzia Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kwa Sh3,600 kwa gunia moja la kilo 90. Hata hivyo, serikali ilikuwa ikinunua mahindi kutoka kwa wakulima kwa Sh3,200 kwa gunia moja la kilo 90. Hii ina maana kuwa wafanyabiashara walikuwa wakipata faidi ya Sh400 juu ya bei mbayo wakulima walikuwa wakilipwa.

Baadaye serikali ilianza kuuza mahindi hayo kwa bei nafuu ya Sh2,300 kwa gunia moja la kilo 90 kwa wasagaji chini ya mpango ambapo bei ya unga ilipunguzwa hadi Sh90 kwa paketi moja ya kilo mbili.

Mpango huo ambao ulianza Julai 2017 na kusitishwa Oktoba 30, uliigharimu serikali Sh6 bilioni.

“Japo tulipoteza mapato kwa kuhusu uagizaji wa mahindi bila kulipiwa ushuru, tulifaulu kutoa afueni kwa wananchi kwa kuweza kupunguza bei ya unga kutoka Sh200 hadi Sh90 kwa paketi ya kilo mbili,” akasema Bw Gaichuhie.

You can share this post!

Ruto avitaka vyuo vifunze kozi zinazowiana na Ajenda Nne Kuu

RIPOTI MAALUM: Echesa taabani kuagiza picha zake za ngono...

adminleo