Sera za Ruto tamu kwa maneno lakini chungu kwa raia
KATIKA kipindi cha karibu miaka mitatu ya uongozi wa Rais William Ruto, Wakenya wameshuhudia mabadiliko mengi ya sera za kiuchumi na kijamii ambazo serikali imekuwa ikitangaza kwa mbwembwe kama njia ya kufufua taifa.
Hata hivyo, hali halisi kwa mwananchi wa kawaida ni tofauti kabisa na kauli za viongozi. Huku Rais na washirika wake wakihubiri matumaini, ripoti kutoka Shirika la Taifa la Takwimu (KNBS) na maisha ya kila siku mitaani zinaonyesha kuwa sera hizi ni tamu kwa maneno lakini sumu kwa maisha ya Wakenya.
Rais Ruto anasema, “Kenya itajengwa na Kenya kwa kutumia ushuru wetu.” Lakini takwimu za KNBS zinaonyesha kuwa gharama ya maisha imeongezeka kwa kasi. Bei ya unga, mafuta ya kupikia na usafiri zimepanda kwa wastani wa asilimia 8 hadi 12 kwa mwaka 2024.
Katika hali ya kushangaza, anapohubiri kupunguza matumizi ya serikali na kubana matumizi ya umma, Rais Ruto ameongeza idadi ya washauri wake wanaofyonza zaidi ya Sh1 bilioni kwa mwaka. Aidha, aliahidi kutokopa ilhali ameongeza deni kwa zaidi ya Sh6 trilioni kwa chini ya miaka mitatu akiwa uongozini.
Wakenya wanahoji serikali inayodai kuwa haina pesa, inatumia mamilioni kulipa washauri huku ikisema haina pesa za kuongezea mishahara madaktari, wauguzi na walimu.
Katika sekta ya ajira, ahadi ya ajira milioni moja kwa mwaka haijatimilika. Badala yake, vijana wengi wamebaki bila ajira, huku ajira zilizopo zikiwa za muda mfupi, zisizo na mikataba wala marupurupu ya msingi huku sera za kiuchumi zikifanya wawekezaji kuhepa Kenya.
Ripoti ya KNBS inasema uchumi ulikua kwa asilimia 4.7 mwaka 2024 kutoka asilimia 5.6 mwaka 2023 — kiwango duni kulinganisha na matarajio. Sekta kama ujenzi, kilimo, na viwanda zimeathirika vibaya na kuporomoka kwa uwezo wa wananchi kutumia pesa.
Katika afya, huduma zimedorora, kuna uhaba wa dawa, migomo ya wahudumu wa afya, na ubora wa huduma umeporomoka. Watoto na wazee wanakosa matibabu kwa sababu ya gharama mpya zisizoeleweka.
“Tofauti kati ya kauli za serikali na uhalisia wa maisha ya wananchi ni kubwa. Ripoti za KNBS zinathibitisha kuwa hali ni mbaya kuliko inavyosemwa hadharani. Ni wakati wa kuhoji sera hizi, si kwa kauli tamu bali kwa matokeo halisi kwa raia wa kawaida,” asema mwanauchumi Charles Ouko.
Anasema katika kile kinachoonekana kinyume na hali halisi nchini, serikali ya Rais William Ruto imekuwa ikidai inatekeleza sera mbalimbali zinazolenga kufufua uchumi na kuboresha maisha ya Wakenya.
“Lakini licha ya lugha tamu na maelezo ya kuvutia kutoka kwa viongozi wa serikali kuhusu sera zake, raia wengi wanalia kwamba sera hizi ni mzigo usiobebeka. Ni sera tamu kwa maneno, lakini sumu katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Sera za utawala wa Kenya Kwanza kuhusu ushuru, leba, uchumi, afya, na elimu zimeathiri vibaya raia,” asisitiza.
Sera ya serikali ya ushuru hasa wa nyumba za bei nafuu inaumiza wafanyakazi. Serikali inatetea mpango huo wa nyumba huku ripoti zikionyesha Wakenya hawana haja nazo na kwamba kazi inazodai inalenga kuunda ni hewa.
Katika upande wa ajira, licha ya ahadi ya kutengeneza nafasi milioni moja kwa mwaka, hali imezidi kuwa mbaya. Wafanyakazi wengi wako kwenye ajira zisizo na mikataba ya kudumu, huku vijana wakihangaika mitaani au kutafuta kazi za kijungujiko.
Ufadhili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu umegeuzwa kuwa mikopo ya bei ya juu ambayo wanafunzi wengi hawawezi kumudu.
Licha ya Rais kusema Kenya ni ya sita kwa uchumi unaokua kwa kasi ulimwenguni Wakenya wengi hawahisi ukuaji wowote.
“Wanaona maisha yao yakizidi kuwa magumu huku viongozi wakihubiri matumaini bila uhalisia. Serikali inaweza kuwa na nia njema, lakini utekelezaji wa sera bila kuzingatia hali halisi ya wananchi ni sawa na kupaka sukari kwenye sumu,”
Ripoti za hivi karibuni kutoka kwa Shirika la Taifa la Takwimu (KNBS) zinaonyesha tofauti kubwa kati ya ahadi za viongozi na hali halisi ya maisha ya wananchi.
Kulingana na ripoti ya KNBS, uchumi wa Kenya ulikua kwa asilimia 4.7 mwaka 2024, ukilinganishwa na asilimia 5.6 mwaka 2023. Hali hii inatokana na kushuka kwa sekta muhimu kama ujenzi na uchimbaji madini, ambazo zilipungua kwa asilimia 2.0 na 11.1 mtawalia.
Hali hii inaonyesha kwamba sera za serikali hazijafanikiwa kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wengi.
Ripoti za KNBS zinaonyesha kuwa ongezeko la bei za bidhaa muhimu, kama vile chakula na usafiri, limeendelea kuwa mzigo kwa wananchi.
Kwa mfano, bei ya unga wa mahindi iliongezeka kwa asilimia 7.0, huku bei ya mafuta ya taa ikiongezeka kwa asilimia 0.6 Hali hii inaonyesha kuwa sera za ushuru za serikali hazijaleta manufaa kwa wananchi wa kawaida.