Makala

Serikali yatetea kuachilia jeshi kukabili GEN Z

Na COLLINS OMULO March 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UTAWALA wa Rais William Ruto umetetea uamuzi wake wa kutuma maafisa wa jeshi kukabili raia wakati wa maandamano ya Gen Z Juni 2024, ukisema nchi ilikuwa katika hatari.

Haya yanajiri huku serikali ikikanusha ripoti za uwezekano wa mapinduzi ya kijeshi mwaka jana, ikitaja habari hizi kama za uongo, zisizo sahihi, na zisizo na msingi wowote.

Akijibu maswali katika Seneti Jumatano (Machi 19, 2025), Waziri wa Ulinzi, Bi Soipan Tuya, alikabiliwa na maswali magumu kuhusu ushiriki wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) katika masuala ya usalama wa ndani.

Seneta wa Kisumu, Tom Ojienda, alimshinikiza waziri kueleza ni wakati gani ambapo KDF inaruhusiwa kuingilia kati masuala ya usalama wa ndani hasa kuhusiana na maandamano ya Gen Z.

Seneta huyo alitaka ufafanuzi kuhusu vigezo vinavyotumika kuamua kushindwa kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kudhibiti hali ya machafuko ya ndani, na hivyo KDF kuhitajika kuingilia kati.

“Ni wakati gani inachukuliwa kuwa ni sawa kwa KDF kuingilia kati pale ambapo kuna tishio halisi na NPS inakosa uwezo wa kudhibiti hali hiyo?” aliuliza Seneta Ojienda.

Akijibu, Waziri Tuya alieleza kuwa KDF huingilia kati vitisho vya ndani kusaidia NPS.

Kwa hivyo, alisema kuwa kutumwa kwa wanajeshi mnamo Juni 25, 2025 kulilenga kusaidia NPS kama ilivyo kwa majukumu mengine ya KDF, lakini hatua hiyo haikuhitaji idhini kutoka kwa Bunge la Kitaifa kwanza.

“Ingawa jukumu la msingi la usalama wa ndani ni la mashirika mengine maalum kama NPS na Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS), pale ambapo kuna vitisho vya ndani dhidi ya uhuru na mamlaka ya Kenya, KDF inaweza kupelekwa,” alisema Bi Tuya.

Seneta wa Kitui, Enock Wambua, alimsukuma zaidi waziri huyo kutaka kujua ni kikosi gani cha KDF kilitumwa barabarani kutuliza ghasia na ikiwa tangazo la serikali lililoruhusu kupelekwa kwa wanajeshi limeondolewa.

“Ningependa kujua kutoka kwa waziri, ni kikosi gani cha KDF kilichopelekwa barabarani Julai 2024? Na pia, tangazo la serikali lililowaruhusu wanajeshi kuingia barabarani, je, limefutwa au linadumu milele?” aliuliza Naibu Kiongozi wa Wachache katika Seneti.

Akijibu, Waziri Tuya alisema kuwa vigezo vya kutumwa kwa wanajeshi viko wazi na kulikuwa na matangazo mawili ya serikali yaliyotolewa kufafanua upeo, muda, na mipaka ya operesheni hiyo ya KDF.

“Sitazungumzia kuhusu kikosi kilichopelekwa kwa kuwa hiyo ni taarifa ya operesheni. Lakini nataka kuhakikishia nchi kuwa maamuzi ya kutumwa kwa wanajeshi hayafanywi kiholela bali ni kwa makini,” alisema.