Mke anafakamia mlo, hana adabu tukiwa mezani
Mke wangu hana adabu za mezani wakati wa kula. Huongea akitafuna chakula, tena anatafuna kwa sauti. Nimejaribu kumzungumzia lakini haelewi. Nifanyeje?
Itabidi umwambie ukweli kuhusu hisia zako na pia umfunze tabia njema mezani kwa upole. Unapofanya hivyo isionekane kana kwamba unamdharau.
Demu wangu mfiadini, anaona tu mbinguni!
Nimekuwa nikimchumbia mwanadada ambaye anapendeza kweli. Huu ni mwezi wa sita sasa tangu tujuane. Lakini amenza kunishangaza. Amezamia sana masuala ya dini kiwango kwamba hata mawasiliano amekatiza. Naomba usaidizi.
Sio vibaya kujitosa katika dini. Ila naye anafaa kuelewa kwamba pia kuna mambo mengine maishani. Zungumza naye ili ujue ukweli.
Ni mrembo kweli kweli ila muongo ajabu!
Kwa miezi kadhaa sasa nimekuwa katika uhusiano na binti mrembo sana, hata tumewazia kuoana. Lakini kuna jambo lanikera; hasemi ukweli. Hakuna wakati hata mmoja ametimiza ahadi. Nitaweza kweli kumvulimia?
Uhusiano unafaa kuwa na uaminifu, lazima wahusika waseme ukweli. Uongo katika uhusiano utakuwa tatizo kubwa na huenda msidumu pamoja. Chaguo ni lako!
Nimempenda mwanadada fulani, tatizo ni kwamba amenizidi umri
Niko na umri wa miaka 30. Kuna demu wa miaka 36 nimekuwa nikirushia ndoano. Sote tuna taaluma nzuri na hakuna aliye katika ndoa. Ninahisi anatosha kuwa mke wangu. Tatizo ni kwamba hanitaki eti kwa sababu amenizidi umri.
Dhana kuwa mwanamke katika uhusiano au ndoa sharti awe mchanga kuliko mwanamume, imepitwa na wakati. Ikiwa mnapendana na kuheshimiana, basi hakuna kosa hapo. Jaribu kumshawishi.