Nimetafuta wa pembeni maana simpendi mume wangu. Nishauri
NIMEOLEWA na nina watoto wawili. Nina mpango wa kando na mwanamume ambaye pia ana familia. Niliamua kwenda nje baada kugundua kuwa simpendi mume wangu. Nilikosea?
Sielewi ni kwa nini umeamua kuishi maisha ya hadaa. Kama humpendi mume wako ina maana kuwa mnapoteza wakati katika ndoa bandia ingawa yeye hajui. Mwambie ukweli muachane.
Kazi inamshinda!
HUU ni mwaka wangu wa pili katika ndoa. Maisha yamekuwa mazuri lakini ghafla mume wangu ameanza kulemewa na wajibu wake. Mara nyingi nikimtaka husema amechoka. Ninashuku ana mpango wa kando. Nishauri.
Mambo ya chumbani yanahitaji mtu kuwa katika hali nzuri kimwili na kiakili. Maisha ya sasa yana changamoto nyingi ambazo zinaweza kuathiri vibaya mwili na mawazo. Shauriana na mume wako ujue hasa tatizo lake kisha mtafute namna ya kulitatua.
Amenifungulia roho
JIRANI yangu wa karibu mtaani ni mwanamke aliye na mtoto aliyezaa na mpenzi wake wa zamani. Tumekuwa marafiki tu na juzi alifungua moyo wake akaungama kuwa ananipenda. Nishauri.
Mwanamke huyo ametangaza mapenzi yake kwako. Uhusiano wa kimapenzi hutokana na wawili kupendana. Jibu lako kwake litategemea iwapo wewe pia unampenda. Kazi kwako.
Yuko tayari kunioa ili kuthibitisha penzi lake
KUNA mwanamume tunayefanya kazi pamoja ambaye ananiambia ananipenda. Nimemwambia athibitishe kweli kuwa ananipenda na akaniambia yuko tayari kunioa. Je, hilo linatosha?
Ahadi inaweza kutimizwa ama kuvunjwa. Mnaweza kupendana leo kisha mmoja wenu abadili nia baada ya muda. Kama wewe pia unampenda, kubali ombi lake. Ndoa kati yenu itategemea mwelekeo wa uhusiano wenu.