Makala

Sharrif Nassir akikohoa, pwani ilikuwa ikishika homa

Na KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK December 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

SHARRIF Nassir bin Taib alikuwa mwanasiasa mwenye sauti zaidi katika Mkoa wa Pwani, na pengine hata nchini Kenya, wakati wa utawala wa Rais Daniel arap Moi.

Mbunge huyo wa Mvita aliyehudumu kuanzia 1974 hadi 2002 alijulikana kwa kutoa maoni yake kwa lolote na kila kitu chini ya jua. Machoni mwake, Moi alikuwa muweza  yote, wa pili baada ya mungu.

Nassir hata alitoa tahadhari na kuwakumbusha waliompinga Rais kwamba chama cha kisiasa cha KANU kingetawala kwa miaka 100.

Kwa hakika, anajulikana kwa matamshi ambayo wengi hufikiria mara nyingi yalionyesha mawazo rasmi ya waliokuwa mamlakani. Alichukuliwa kama mfalme kamili wa kisiasa huko Mombasa na sehemu kubwa ya mkoa wa Pwani.

Kigogo wa Kanu Mombasa

Hakika, magazeti ya Kenya mara nyingi yalimtaja kama ‘kigogo wa KANU Mombasa’, kwa kurejelea ushawishi wake mkubwa  kisiasa. Kwa wakosoaji wake ndani na nje ya KANU, Nassir aliwakilisha uhafidhina wa Kanu.

Kwa mfano, mnamo Machi 1999, alikuja na pendekezo utata la Moi kubaki mamlakani zaidi ya mihula yake miwili ya miaka mitano kikatiba. Wakati huo, Moi alikuwa akitumikia muhula wake wa pili na wa mwisho ofisini.

Nassir, mwenye asili ya Kiarabu, alizaliwa Mombasa kama walivyokuwa wazazi wake. Babake Shariff Abdulla Taib, alihamia Lamu, lakini Nassir  alirejea Mombasa kwa masomo yake ya msingi katika Shule ya Msingi ya Serani (zamani  Arab Boys School) kabla ya kuhudhuria Shule ya Upili ya Shimo la Tewa ambako alifanya mtihani wa msingi  na wa upili wa Cambridge.

Alipomaliza masomo yake, alifanya kazi kama karani, akipanda cheo na kuwa Meneja katika Kampuni ya Maritime ya Afrika Mashariki.

Nassir alijiunga na chama cha Coast People’s Party (CPP) kilichoongozwa na Ronald Ngala kabla ya uhuru. Kisha akahamia Kenya African Democratic Union (KADU) ambayo Ngala alikua Katibu Mkuu baada ya CPP kuvunjwa. Wakati huo, KADU kilikuwa chama maarufu zaidi cha kisiasa katika eneo la Pwani.

Kiti cha ubunge cha Mvita

Baada ya uhuru, viongozi hao wawili, Nassir na Ngala, walivunja KADU na kujiunga na KANU, na wakahudumu kama Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti wa Tawi la Mombasa mtawalia.

Hatimaye Nassir alitwaa wadhifa wa Mwenyekiti wa Tawi baada ya kifo cha Ngala mwaka wa 1972. Baadaye aligombea kiti cha ubunge cha Mvita na kumshinda Mohamed Jahazi ambaye alikuwa amejiimarisha kama nguzo katika siasa za Mombasa.

Kabla ya kugombea ubunge, Nassir aliwahi kuwa Diwani wa Wadi ya Makadara, Mombasa.

Ni muhimu kutambua kwamba wakati wa vita vikali vya urithi wa urais vilivyotangulia kifo cha Rais mwanzilishi Jomo Kenyatta, wanasiasa kadhaa walijihusisha na mirengo ya KANU iliyoegemea hima Makamu wa Rais Moi au wanasiasa wa Mlima Kenya chini  muungano wa Chama cha Gikuyu, Embu na Meru (GEMA).

Vuguvugu la cha ‘Change-the-Constitution’ lililoongozwa na Mbunge wa Nakuru Kihika Kimani lilikuwa kali sana hivi kwamba lilichochea sehemu za nchi dhidi ya Moi.

Nassir alikuwa miongoni mwa walioegemea upande wa Moi. Wengine walikuwa Mwanasheria Mkuu Charles Njonjo na Mawaziri Mwai Kibaki, Julius Kiano, G.G. Kariuki na Stanley Oloitiptip.

Wakati wa malipo kwa Nassir

Kwa hivyo ulikuwa wakati wa malipo kwa Nassir na wafuasi wengine watiifu wakati Moi alipoingia mamlaka mnamo Agosti 1978.

Kwa hivyo, nafasi ya Nassir kama mshirika wa Moi iliimarishwa. Nassir aliharakisha kumpendekeza Moi kama Rais mara tu baada ya kifo cha Kenyatta.

Licha ya kuwa karibu na Moi kwa miaka mingi, Nassir hakuteuliwa Waziri hadi baadaye katika urais wa Moi.

Alipata uteuzi wake kamili wa kwanza wa uwaziri mnamo Februari 1998 kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Desemba 1997, na hivyo kuungana na Hussein Maalim Mohamed kama Mawaziri pekee Waislamu katika Baraza la Mawaziri.

Hata hivyo, Nassir aliwahi kuwa Waziri Msaidizi katika Wizara nyingi, zikiwemo Habari na Utangazaji, Mazingira na Maliasili, Ardhi na Makazi, Kazi, Biashara na Viwanda, Fedha, Mwongozo wa Kitaifa na Masuala ya Siasa, na Mambo ya Ndani na Urithi wa Taifa.

Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri

Kufuatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri Februari 1999 ambapo Shariff aliteuliwa waziri wa Masuala ya Ndani, Moi alisema mabadiliko hayo yalilenga “kuondoa ukiukaji wa taratibu za utoaji wa zabuni na ununuzi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.” Mawaziri Wasaidizi wa Nassir walikuwa Marere Wamwachai na John Marimoi.

Watu wengi wanahusisha kusita kwa Moi kumteua Nassir kuwa waziri na kiwango chake cha chini cha elimu; Kiingereza chake hakikuwa kizuri kama Kiswahili chake.

Uteuzi wake, hata hivyo, ulikuwa zawadi kwa Nassir kwa jukumu lake dhahiri katika kuinua ustawi wa chama tawala cha KANU huko Mombasa.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA