SHINA LA UHAI: Huenda ukapima ubongo wa mtoto angali tumboni
Na LEONARD ONYANGO
AKINA mama wajawazito huenda wakatumia simu kupima watoto wao tumboni kubainisha ikiwa ubongo una dosari au la.
Watafiti nchini Australia wameanza shughuli ya kufanyia majaribio teknolojia inayoaminika kuwa inaweza kutambua afya ya ubongo wa mtoto aliye tumboni, kulingana na shirika la habari la China, Xinhua.
Wizara ya Afya ya Watoto na Vijana itaongoza utafiti huo utakaohusisha jumla ya wanawake wajawazito 3,000.
Watoto walio tumboni watapimwa mara moja kila baada ya wiki mbili ili kubaini mapigo ya bongo zao.
Mtoto ambaye ubongo wake utapatikana na mapigo tofauti na wenzake atafanyiwa uchunguzi zaidi maabarani.
Watafiti hao wanaamini kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa na matatizo ya ubongo itapungua kwa kiasi kikubwa endapo utafiti huo utafaulu.
“Mradi huu ni ithibati kwamba teknolojia itafanya makuu katika kuboresha afya,” akasema waziri wa Afya wa jimbo la West Australian (WA) Roger Cook.
Baadaye watafiti hao watatengeneza programu (app) ya simu ambayo itafunzwa namna ya kutofautisha mapigo ya ubongo ulio sawa na ulio na dosari.
Wataalamu wanasema kuwa teknolojia huenda ikawafaa watu wanaoishi maeneo yaliyo mbali na vituo vya afya.
“Teknolojia hii itasaidia kutambua watoto walio na matatizo ya ubongo ili kuwatibu mapema,” akasema Cook.
Tayari wataalamu wanatumia mapigo ya ubongo kubaini dosari ya ubongo (cerebral palsy).
Watafiti nchini Australia wanaamini kwamba wanaweza kutumia teknolojia sawa kubaini matatizo mengineyo ya ubongo.
Kituo cha Kutafiti Maradhi (CDC) kinakadiria kuwa kati ya watoto 320 wanaozaliwa, mmoja ana tatizo la ubongo.
Ni nini kinasababisha matatizo ya ubongo mtoto anapokuwa tumboni?
Wataalamu wanasema kuwa ukosefu wa madini muhimu ya chuma na vitamini D, kunaweza kusababisha ubongo wa mtoto kuwa hafifu.
Wanawake wajawazito pia wanashauriwa kujiepusha na matumizi ya dawa kiholela bila kupata ushauri kutoka kwa daktari.
Dawa za kawaida kama vile aspirin, kwa mfano, zinaweza kusababisha damu kuvuja kwenye ubongo wa mtoto aliye tumboni.
Utafiti uliochapishwa katika jarida la matibabu la Lancet, ulibaini kuwa mama mjamzito anapokumbwa na mzongo wa mawazo mara kwa mara anaweza kuathiri afya ya ubongo ya mtoto. Matumizi ya tumbako, mvinyo na dawa nyinginezo za kulevya zinaathiri ubongo wa mtoto aliye tumboni.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Statens Serum ya Denmark ulibaini kwamba uvutaji wa sigara pia unaathiri macho ya mtoto aliye tumboni. Watoto ambao mama zao wanavuta bangi wakati wa ujauzito pia wanaathirika kiakili.
Akili punguani
Pombe hupitia katika kitovu kutoka kwa mama na kuingia kwa mtoto ambapo humfanya kuwa na akili punguani, kukosa kumbukumbu, kuwa na kichwa kidogo, kati ya matatizo mengineyo.
Hewa chafu pia inaathiri ubongo wa watoto. Ugonjwa wa kaswende na kisonono pia husababisha matatizo ya ubongo, mifupa, ngozi na ini kwa mtoto aliye tumboni.
Kulingana na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef), ubongo wa watoto hukua kwa kasi zaidi kati ya kipindi akiwa tumboni na umri wa miaka miwili baada ya kuzaliwa.
Ubongo wa mtoto akiwa na miezi mitano tumboni hulingana na haragwe. Anapofikisha miezi tisa ya kuzaliwa, ubongo huonekana sawa na ule wa mtu mzima. Kati ya kipindi cha ujauzito na umri wa miaka miwili mtoto baada ya kuzaliwa, anahitajika kupata chakula cha kutosha kuwezesha ukuaji wa ubongo.