SHINA LA UHAI: Ijue saratani ya damu na inavyosambaa
Na BENSON MATHEKA
HUKU idadi ya watu wanaougua saratani ikiendelea kuongezeka, imebainika kuwa inachukua madaktari muda kuitambua na baadhi hupatia wagonjwa matibabu ya maradhi tofauti.
Mfano mzuri ni kansa iliyosababisha kifo cha Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Safaricom Bob Collymore.
Ingawa alikuwa akiugua Acute Myeloid Leukemia (AML), mojawapo ya aina nne za saratani ya damu, madaktari walitangulia kumweleza kwamba alikuwa na uhaba wa vitamini mwilini.
Licha yake kutembelea hospitali kubwakubwa nchini zilizo na wataalamu na vifaa bora kabla ya kwenda ng’ambo, haikugunduliwa mapema kwamba alikuwa akiugua saratani jambo ambalo wataalamu wanasema limechangia vifo vingi vinavyotokana na maradhi haya.
Akiongea katika kipindi kimoja cha runinga baada ya kurejea nchini kutoka ng’ambo alikokuwa akitibiwa, Bob alisema mara ya kwanza alipotafuta matibabu, alifahamishwa kwamba alikuwa na uhaba wa vitamin D mwilini badala ya ugonjwa uliosababisha kifo chake.
“Nilikuwa nikijihisi mgonjwa kwa muda, uchovu na joto jingi mara kwa mara, hali ilizidi kuwa mbaya hivi kwamba sikuweza kuhudhuria hafla za kikazi,” alisema.
Baadaye alianza kupata dalili za mafua, kutetemeka mwili na maumivu makali ya mifupa miguuni chini ya goti. Ni wakati huo madaktari walipomfahamisha kwamba alikuwa na upungufu wa Vitamin D.
Alieleza kuwa hakuridhishwa na maelezo ya daktari huyo na akatafuta ushauri zaidi kutoka kwa Dkt David Silverstein katika Nairobi Hospital.
Kulingana naye, ilichukua vipimo 30 tofauti vya damu kwa gharama ya Sh100,000 kabla ya Dkt Silverstein kumtarifu alifaa kwenda ng’ambo kwa dharura kuchunguzwa zaidi. Ni akiwa ng’ambo ambapo madaktari waligundua kwamba alikuwa na saratani ya damu.
Kulingana na Dkt Andrew Odhiambo, mtaalamu wa maradhi ya saratani, kutogunduliwa mapema au kukosa kutibiwa kwa maradhi tofauti mapema husababisha vifo.
Hata hivyo, anaeleza kuwa gharama ya kupimwa na kutibiwa saratani hutegemea na aina inayompata mtu.
Maradhi haya hayabagui tajiri wala maskini ila masikini ndio hulemewa zaidi, jambo ambalo Bob aliungama.
“Nilijiuliza, kama singekuwa mfanyakazi wa Safaricom na Vodacom je, ningemudu; kusema kweli ingekuwa vigumu kwangu,” akasema wakati wa mahojiano hayo.
Saratani ya damu au Leukemia ni hali ambayo mwili unatengeneza seli nyingi sana nyeupe za damu, kuliko kiwango ambacho kinatakiwa mwilini. Seli hizi hutengenezwa na uvimbe (tumour) ambao hukua ndani ya mifupa ya kutengeneza damu.
Wataalamu wa saratani wanasema kila aina ya Leukemia hutambuliwa kulingana na aina ya seli za damu zinazoathiriwa na kwa kasi ambayo ugonjwa huo huenea katika mwili.
Bob alifichua kwamba alikuwa akiugua Acute Myeloid Leukemia, kumaanisha kwamba ilienea kwa haraka na kuwa mbaya zaidi.
“Ugonjwa wowote huwa unaorodheshwa kuwa ‘Acute’ ikiwa unaenea au kusambaa mwilini haraka. Hii ni kumaanisha unaweza kuhisi dalili za ugonjwa na baada ya muda mfupi uwe umeenea na kukomaa mwilini. Katika hali hii huwa ni vigumu kuudhibiti,” asema Dkt Absa Shah, mtaalamu wa saratani katika Cancer Center, hospitali ya M.P Shah.
Anaeleza kwamba saratani hii huwa inaanza katika seli nyekundu za damu au chembechembe nyingine za damu. Kuna aina mbili za satarani ya damu ambazo ni ‘Acute’ na ‘Chronic’ Leukemia.
‘Acute’ Leukemia huenea kwa haraka na kusababisha mwili kuunda seli ambazo hazijakomaa ndani ya uboho (bone marrow) hivyo kuzuia mifupa kutengeneza seli zingine za kawaida. Kwa aina hii ya saratani ya damu, seli huzaana na kukusanyika katika uboho na kupunguza uwezo wake wa kutoa seli za damu zenye nguvu.
Kuna aina ya saratani ya damu ambayo huchukua muda kuenea na inafahamika kama ‘Chronic’ Leukemia ambayo husababishwa na seli nyeupe za damu ambazo zimekomaa.
“Kuna aina tofauti za Leukemia na daktari akigundua aina ambayo mgonjwa anaugua, huwa anaweza kupanga matibabu bora na yanayofaa,” aeleza.
Mtaalamu wa saratani katika Nairobi Hospital Profesa Othieno Abinya, anasema mtu akiugua Chronic Myeloid Leukemia, anaweza kuishi maisha marefu akitumia dawa ambazo huwa ni ghali mno. Bei ya dawa hizo ambazo mtu anafaa kutumia kila siku ni kati ya Sh200,000 na Sh400,000. Hata hivyo, Nairobi Hospital kwa ushirikiano na wakfu wa Max Foundation imekuwa ikitoa dawa hizi bila malipo.
Profesa Abinya anasema kwamba matumaini ya kuishi ya wanaougua Acute Myeloid Leukemia ni finyu mno hasa kwa watu wa umri mkubwa. “Matibabu huwa magumu na yanaweza kuua mgonjwa. Mgonjwa pia anaweza kupata maradhi mengine kwa haraka na yasababishe mauti,” asema.
Kansa ya aina hii ni adimu sana na hupata mtu mmoja kati ya watu 100,000 nchini wengi wakiwa wanaume. Kulingana na Dkt B. S Menon, mtafiti na mtaalamu wa saratani katika kituo cha Cancer Center, anasema wanawake wana jeni ambazo huwapa kinga zaidi na pia walio na aina ya damu O sio rahisi kupata saratani hii.
Kulingana na wataalamu, watoto pia wanaweza kupata saratani ya damu. “Kuna aina za Leukemia ambazo huwapata watoto na aina nyingine huwapata watu wazima,” aeleza.
Matibabu ya saratani hii hutegemea aina yake na pia hali ya mgonjwa. Dalili zake pia huwa zinategemea aina ya Leukemia, asema Dkt Shah.
Dalili za Leukemia
•Uchovu wa mara kwa mara na mwili kukosa nguvu
•Kuhisi baridi na homa
•Kuugua mara kwa mara na kupunguza uzani wa mwili
• Kuvimba kwa ini na wengu(spleen)
• Kutokwa na damu kwa haraka
• Kutokwa na damu mapuani mara kwa mara.
• Kuumwa kichwa, kupata kizunguzungu, kichefuchefu na kutapika
• Kupata alama ndogo nyekundu mwilini
• Kutokwa na jasho jingi hasa usiku na maumivu ya mifupa.
Licha ya dalili hizi, wataalamu wanasema inaweza kuchukua muda saratani kugunduliwa kwa sababu zinafanana na za maradhi mengine.
Dalili hizi zinaweza kupuuzwa kwa sababu zinafanana na za mafua na maradhi mengine ya kawaida na sio rahisi kugunduliwa mtu anapopimwa damu kuchunguzwa iwapo anaugua magonjwa mengine.
Kila mtu anaweza kupata Leukemia na wanasayansi wanasema sawa na aina nyingine za saratani, kinachosababisha hakijulikani hasa.
Hata hivyo, wanasema inaweza kuhusishwa na aina ya jeni na mazingira. Watu ambao wamewahi kupata matibabu ya saratani huwa katika hatari ya kupata aina tofauti za Leukemia.
Wataalamu wanasema kote ulimwenguni kati ya asilimia 5-10 ya visa vya saratani vinahusishwa na jeni kumaanisha mtu anaweza kurithi. Aidha asilimia 90-95 vinahusishwa na mazingira na mitindo ya maisha kama vile uvutaji wa sigara, lishe, pombe na kukosa kufanya mazoezi ya mwili.
Kati ya asilimia 20 na 30 ya vifo vinavyosababishwa na kansa ni kwa sababu ya matumizi ya tumbako, asilimia 30-35 vinatokana na lishe na asilimia 15-20 vinasababishwa na maambukizi kwa mfano kwa kukaa karibu na mtu anayevuta sigara.
Baadhi ya kemikali zinazotumiwa viwandani na uvutaji wa sigara pia zinaweza kusababisha baadhi ya aina za saratani ya damu kama vile Acute Myelogenous Leukemia.
Wataalamu wanasema kwamba watu wanaotoka familia ambazo kunao wamewahi kuugua maradhi haya, huwa katika hatari kubwa ya kupata saratani hii.
Mikakati ya serikali kupambana na kansa
Kulingana na mikakati ya serikali ya kukabili janga la saratani kati ya mwaka 2017 na 2022, wizara ya Afya inaorodhesha awamu tano muhimu;
1. Awamu ya kwanza inahusisha kuzuia, kutambuliwa mapema na uchunguzi.
2. Ya pili ni kugunduliwa mapema, kusajiliwa kwa visa vya saratani na kuzifuatilia.
3. Awamu ya tatu inahusisha matibabu na kutunza waathiriwa.
4. Nne inahusu ushirikiano ili kudhibiti saratani.
5. Na tano kutathmini na utafiti.
Viwango vya maambukizi ya saratani
Ripoti ya wizara ya Afya inasema ugonjwa wa saratani ni wa tatu kwa kuua watu wengi nchini Kenya tangu 2012 baada ya maradhi ya kuambukizwa na matatizo ya moyo.
Mnamo 2012, watu 37,000 walipata saratani na 28,500 waliuawa na ugonjwa huo humu nchini.
Kulingana na ripoti ya shirika la kimataifa la kutafiti saratani, ni watu 47, 887 waliopata kansa nchini Kenya 2018 na miongoni mwao 32,987 walifariki.
Kati ya watu wapya walioambukizwa, wanawake walikuwa 28, 688 na wanaume walikuwa 19, 199 kuonyesha kuwa wanawake wanakabiliwa na hatari ya kuuawa na kansa kuliko wanaume.
Ripoti inaonyesha visa vya kansa ya matiti vilikuwa 5,985 ongezeko la asilimia 12.5 na kansa ya sehemu ya uzazi vilikuwa 5,250 ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.
Miongoni mwa wanaume, kansa ya kibofu iliongoza kwa kuua watu wengi huku visa vipya 2,864 vikiripotiwa ikiwa ni ongezeko la 14.9. Ilifuatiwa na saratani ya koo visa vipya 2,384 vikiripotiwa ambavyo viliongezeka kwa asilimia 12.4.
Gharama ya matibabu
Gharama ya matibabu ya saratani nchini ikiwemo hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta jijini Nairobi iko juu sana.
Kulingana na ripoti za wataalamu wa saratani, inagharimu kati ya Sh172, 000 na Sh759,000 kutibu saratani ya sehemu ya uzazi nchini na kati ya Sh672,000 na Sh1.25 milioni ikiwa mgonjwa atafanyiwa upasuaji.
Kutibu saratani ya matiti kunagharimu kati ya Sh175, 000 hadi Sh1.98 milioni na gharama hii inaweza kuongezeka hadi Sh2.8 milioni kwa kutegemea hali ya matibabu anayohitaji mgonjwa.
Kwa wanaume wanaogua kansa ya kibofu matibabu hugharimu kati ya Sh138, 000 na Sh1.21 milioni huku saratani ya koo ikigharimu kati ya Sh1 milioni na Sh126, 000.
Ingawa wataalamu wanahimiza watu kuchukua bima ya afya ili kufadhili matibabu ya saratani, gharama inazidi kulemea wengi.
Mpango wa matibabu bila malipo ambao serikali inafanyia majaribio haufadhili matibabu ya magonjwa sugu kwa sasa na watu wanashauriwa kuchukua bima ya taifa ya afya NHIF.
Takwimu za NHIF mwaka 2018 zinaonyesha kuwa ilitumia Sh1.23 bilioni kufadhili matibabu ya saratani mwaka 2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 11 kutoka mwaka 2017.