SHINA LA UHAI: Watumiaji mihadarati sasa watatambulika kwa kupimwa viganja
Na LEONARD ONYANGO
MIKONO ya watumiaji wa mihadarati huenda sasa ikatumika kama ushahidi kortini baada ya wanasayansi wa nchini Uingereza kutengeneza teknolojia inayotambua watu ambao wamewahi kushika kokeni na heroini.
Kwa kupima mikono, polisi wataweza kutambua watu ambao wamewahi kushika heroini au kokeni hata kama wamenawa.
Teknolojia hiyo pia ina uwezo wa kutofautisha watu waliogusa mihadarati hiyo kwa kusalimiana na watumiaji na wale ambao wamekuwa wakiishika mara kwa mara.
Teknolojia hiyo imetengenezwa na watafiti katika Chuo Kikuu cha Surrey. Watafiti walitumia mikono ya waraibu wa kokeni na heroini waliokuwa wakitafuta huduma za matibabu hospitalini na vituo vya kubadilisha tabia, wakati wa kutengeneza teknolojia hiyo.
Waraibu hao walitakiwa kunawa mikono na maji ya sabuni na kisha wakavalishwa glavu. Mikono yao ilitokwa na jasho ndani ya glovu na kisha jasho hilo likapimwa na wataalamu ndani ya maabara.
“Teknolojia hiyo iliweza kutofautisha watu ambao wametumia kokeni na heroini kwa kipindi kirefu na wale waligusa tu kiajali,” akasema Catia Costa, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Surrey.
Watafiti hao, kupitia ripoti yao iliyochapishwa katika jarida la kitafiti la The Journal of Analytical Toxicology, walisema kuwa teknolojia hiyo inaweza kutumika kutambua waraibu wa mihadarati na hata kunasa walanguzi wa kokeni na heroini.
“Matokeo yanaonyesha kuwa teknolojia hiyo inaweza kumtambua mtu ambaye amekuwa akitumia mihadarati hata baada ya kuosha mikono,” wanasema.
Heroini inatokana na mmea unaofahamika kama Opium Poppy ambao hupatikana katika nchi za Afghanistan, Pakistan, Iraq na Uturuki. Kiasi kikubwa cha shehena ya heroini hupitia Kenya na mataifa mengine ya Afrika Mashariki kuelekea Amerika na Ulaya.
Kokeni hutokana na mmea unaofahamika kama Coca ambao hupatikana kwa wingi nchini Peru, Bolivia, Brazil, Mexico, Columbia na Venezuela. Kenya imetajwa kuwa miongoni mwa mataifa ambapo kokeni hupitishwa kuelekea Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika Kusini.
Kulingana na shirika la kimataifa la International Drugs Policy Consortium (IDPC), heroini ilianza kutumiwa jijini Mombasa kabla ya kusambaa katika maeneo mengine ya nchi kama vile Nairobi.
Inakadikadiriwa kuwa kati ya Wakenya 30,000 na 70,000 wanatumia heroini ambayo imeharamishwa humu nchini.
Ripoti ya Mamlaka ya Kukabiliana na Dawa za Kulevya nchini (Nacada) iliyotolewa mwaka huu, inaonyesha kuwa heroini sasa inatumiwa katika karibu kaunti zote nchini.
Asilimia 11 ya wanafunzi wa shule ya msingi waliohojiwa katika ripoti hiyo walikiri kuwa heroini inauzwa karibu na shule zao.
La kushangaza
Jambo la kushangaza ni kuwa asilimia 11.2 ya wanafunzi wa shule za msingi za vijijini walikiri kwamba heroini inauzwa karibu na shule zao ikilinganishwa na asilimia 9.8 ya wanafunzi kutoka mijini.
Asilimia 3.6 ya wanafunzi hao walikiri kuwa wamewahi kutumia au kuona wenzao wakitumia heroini.
Asilimia 0.9 pia walikiri kuwa wamewahi kutumia kokeni.
Kaunti za Bungoma na Murang’a zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaotumia kokeni kwa asilimia 1.7 na 1.4 mtawalia, kulingana na ripoti hiyo ya Nacada.
Heroini inaweza kudungwa ndani ya mwili kwa kutumia sindano, kuweka puani na hata waraibu wengine huvuta kama sigara.
Huingia ndani ya ubongo kwa kasi na huharibu sehemu za ubongo ambazo huhusika na kuhisi maumivu na raha.
Heroini pia huvuruga mapigo ya moyo, usingizi na husababisha matatizo ya kupumua.
Inapotumiwa kwa muda mrefu, heroini husababisha mtumiaji kuwa mwendawazimu, kupata matatizo ya ini na figo, wanaume kuwa mabwege kitandani na huvuruga hedhi miongoni mwa wanawake.
Kokeni pia hutumiwa sawa na heroini. Unga wa kokeni hutumiwa kupitia puani, kuweka kwenye fizi na wengine huweka ndani ya maji na kujidunga kwa sindano.