Makala

SIHA NA LISHE: Huzioka keki kwa kutumia unga asilia

November 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER CHANGTOEK

UMBALI wa mita 800 kutoka mjini Chuka, nyuma ya shule ya Upili ya Wasichana ya Chuka, Nancy Kendi, 29, hushughulika na utengenezaji wa vyakula mbalimbali kwa kuutumia unga wa nafaka tofauti tofauti.

Yeye huvitengeneza vyakula kama vile keki kutoka kwa unga wa mtama, ndizi, wimbi, na mihogo.

Kendi amekuwa na uchu wa kuvitayarisha vyakula vya sampuli hiyo kwa kuutumia unga ambao wengi huupuuza.

Aghalabu, waja wengi huutumia unga wa ngano kuvitengeneza vyakula kama vile keki, lakini Bi Kendi ameamua kuutumia unga asilia.

Kendi, ambaye ana shahada katika masuala ya usimamizi wa biashara, anasema kuwa unga huo una virutubisho ambavyo ni bora kwa watu, hususan wale ambao ni wakongwe na watoto. Hata hivyo, anasikitika kuwa watu wengi mno hukosa kuutumia unga uo huo, kwa kupuuza tu.

“Ili kutoa fursa kwa watu kula vyakula vyenye virutubisho kwa wingi, katika maeneo yanayokabiliwa na ukame kama Tharaka Nithi, ilibidi nitumie njia za kuvutia, ili kuwafanya wakazi kula hivyo virutubisho vilivyomo kwa vyakula ambavyo vinapatikana kwa urahisi, lakini hupuuzwa sana,’’ anasema Kendi.

Bi Kendi alianza kupika kwa kuutumia unga ambao ni nadra kupatikana, mnamo mwaka 2016, ili kujiepusha na mbinu za ‘kuchosha’ za kupika mathalani; kuchemsha, kupondaponda, na kuchoma.

Mjasiriamali huyo, huzitengeneza chapati za ndizi, keki za ndizi, kaukau za ndizi (banana crisps), keki za bitiruti (beetroot cakes), miongoni mwa vyakula vinginevyo.

Alianza kwa kuvipika vyakula hivyo ili viliwe na aila yake, kisha baadaye akaanza kuviuza kwa wateja wake.

Kendi huununua unga wa nafaka mbalimbali kutoka kwa vikundi tofauti tofauti vilivyosajiliwa rasmi. Baada ya kuununua unga huo, yeye huuchanganya vyema, kabla hajaanza kuutumia.

Anadokeza kwamba watu wengi mno hawana ufahamu kuwa unga asilia unaweza kuboresha afya zao.

Alijifunza jinsi ya kuoka kupitia kwa mikutano iliyokuwa ikiandaliwa na idara ya kilimo ya kaunti hiyo.

Pia, alihudhuria warsha zilizoandaliwa na Shirika la Kilimo na Chakula (FAO), mwezi Februari, zilizokuwa zimeandaliwa katika shamba la Kaguru Farm, katika kaunti ya Meru.

Aidha, Kendi amewahi kupata fursa ya kuonyesha bidhaa zake kwa hadhira, katika mokongamano mengi; kama vile kongamano la ugatuzi lililoandaliwa katika Kaunti ya Kirinyaga na katika lile lililokuwa limeandaliwa mjini Njoro, Kaunti ya Nakuru, mnamo Oktoba 16, 2018, wakati wa kusherehekea siku ya chakula duniani.

Fauka ya hayo, katika jitihada za kuboresha ujuzi wake wa uokaji, Kendi aliamua kujisajili ili awe akipata mafunzo ya ziada kwa kozi ya uokaji mitandaoni.

Anaongeza kuwa chakula na virutubisho husaidia pakubwa kuimarisha afya ya binadamu.

“Aina hizi nyingi za unga zina manufaa mengi. Vyakula hivi humeng’enywa kwa urahisi. Unga huo hupatikana kwa urahisi na si ghali,’’ anafichua.

Wimbi, kwa mfano, huwa na manufaa mengi. Huwa na protini na aina fulani za madini. Pia, huwa na vitamini.

Mitama, nayo, husaidia kurahisisha shughuli ya mmeng’enyo wa chakula tumboni. Huondoa kuvimbiwa tumboni baada ya kukila chakula.

“Husaidia kupunguza athari za maradhi ya kisukari na husaidia kuimarisha afya ya mifupa kwa sababu ina kalisiamu (Calcium). Mitama husaidia kusambazwa kwa madini ya shaba, zinki, chuma, ‘magnesium’, kalisiamu na madini mengine kwa mwili,’’ anasema.

Kwa mujibu wa Kendi, mihogo ina vitamini, madini, na huwa na vitamini C.

Bw Benard Kinoti, mtaalamu wa lishe, ambaye pia ni afisa wa kilimo nyanjani mjini Meru, anasema kuwa unga asilia una manufaa yasiyohesabika.

Anafichua kuwa unga uo huo hauna kuvu ambayo ni sumu, na ni bora kuliko aina yoyote ya unga wa ngano.