SIHA NA LISHE: Jinsi ya kutunza afya yako
Na MARGARET MAINA
KATIKA kujiweka mwenye afya njema au unapotaka kujiweka sawa kwa ajili ya kuonekana mrembo, ni kazi ambayo inahitaji muda na uvumilivu.
Na kwa mwanamke ambaye ana watoto, familia na kazi, anahitaji ukakamavu mkubwa huku akitakiwa kuonekana bomba na mchangamfu.
Inalazimu ajitahidi kutenga muda wake binafsi kwa ajili ya kutunza mwili na afya yake.
Watu wengi hasa wanawake wanapokuwa katika mtawanyiko wa mambo hujisahau kabisa na mara nyingi husahau kuwa wanahitaji kula na kufanya vitu fulani ili kujiweka wenye afya nzuri.
Jaribu yafuatayo
Siku zote hakikisha una tunda kama sehemu ya kifungua kinywa chako. Hii inasaidia kuondoa sumu katika mwili wako na kusaidia kuondoa uchafu uliojiweka kwa namna isiyostahili.
Kunywa maji ya kutosha. Anza kwa kupunguza chai na kahawa kufikia angalau vikombe viwili kwa siku na muda uliobaki kunywa vinywaji ambavyo ni vya mizizi kama jasmine na chamoile tea. Vinywaji hivi katika mfumo wajuisi ni dawa tosha kwa ngozi yako na ili ionekane ya ujana muda wote na isiwe kavu.
Huku umri wako ukiwa unapanda, punguza vyakula vya nafaka na kula zaidi matunda na mbogamboga ili kupunguza uzito.
Hakikisha unatembea vya kutosha na kujinyoosha ili uwe na mwili wa kuvutia, mwembamba na wenye nguvu za kutosha na wa ujana.
Punguza uvutaji sigara na matumizi ya pombe kwani ni vitu viwili vinavyozeesha ngozi kwa kasi.
Ongeza vyakula vya samaki katika chakula chako au aina yake.
Jipatie vitamu vya asili kama asali na raisins.
Kujisikia vyema; huku ni kujipenda mwenyewe. Kama hujipendi huwezi ukavutia.