SIHA, LISHE NA ULIMBWENDE: Manufaa ya ukwaju katika mwili wa binadamu
Na MARGARET MAINA
UKWAJU ni tunda la mkwaju ambalo hupatikana katika maeneo ya kitropiki.
Kwa Kiingereza hujulikana kama tamarind na ambapo jina la kisayansi la mkwaju niĀ Tamarindus indica.
Katika baadhi ya maeneo, ukwaju hutumiwa kama kiungo katika mboga.
Ukwaju una madini ambayo ni muhimu sana kwa afya zetu. Una calcium, vitamini C, copper, phosphorus, madini ya chuma, na magnisium.
Namna ya kuutumia ukwaju
Tengeneza juisi nzuri ya ukwaju. Anza kuitumia kama kiungo katika chakula. Unaweza pia kuyatafuna majani ya mkwaju yenye ladha ya chumvichumvi au kuyakausha majani hayo kivulini na kuweka katika uji, au supu au juisi ya matunda.
Zifuatazo ni baadhi ya faida zitokanazo na matumizi ya ukwaju
Ukwaju husaidia kuongeza uwezo wa macho kuona. Matumizi ya ukwaju, ama kwa kula au kutumia kama juisi huondoa matatizo ya macho na kukufanya uwe na macho yenye afya.
Tunda hili ni muhimu na husaidia wenye ugonjwa wa kisukari kwa sababu ukwaju una viambata muhimu kama polyphenols na flavonoids ambavyo ni madhubuti katika kurekebisha au kusawazisha kiwango cha sukari mwilini na kupunguza vitambi.
Husaidia kwa wenye shinikizo la damu. Hivyo ni muhimu kunywa juisi ya ukwaju mara kwa mara.
Ifahamike kwamba ukwaju hupunguza kiwango kikubwa cha lehemu (cholesterol) mwilini.
Ukwaju una faida kwani pia hutoa mchango muhimu katika kusafisha damu.
Huondoa tatizo la nywele kukatika, na kuzipa mng’aro halisi. Anayetumia tunda hili kwa ajili ya kutunza nywele anafaa kuchemsha ukwaju, kisha kuanza kuyatumia maji yake ambapo anahitajika kuyachanganya na vijiko viwili vya bizari kabla ya kutumia kusafisha nywele kwa njia iliyo taratibu. Mtumiaji akishafanya hivyo anashauriwa kuziache nywele kwa muda wa nusu saa na azioshe kwa maji fufutende.
Ukwaju huboresha mfumo wa mmeng ‘enyo na kuondoa gesi. Anayetumia kupata faida hii anahitaji juisi ya ukwaju.
Manufaa ya mwisho katika makala hii ni kwamba tunda hili husaidia kupunguza uzani na pia kuboresha ngozi ya mtumiaji.