Sina nguvu, sina uwezo asema Guardiola akionekana kukosa suluhu ya matatizo Man City
KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola anaonekana kukata tamaa kuwa huenda hatashinda Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2024-2025.
Guardiola, ambaye anaaminika kumezewa mate na timu ya taifa ya Brazil, ni mmoja wa makocha waliopata mafanikio makubwa katika ulimwengu wa soka.
Anajivunia mataji 14 akiwa na FC Barcelona, saba akiongoza Bayern Munich na 17 akiwa usukani City.
Hata hivyo, Mhispania huyo amepoteza mechi nne mfululizo kwa mara ya kwanza kabisa na kudokeza kuwa wakati umewadia timu nyingine kutawala ligi hiyo ya klabu 20.
Ameshinda EPL mara nne mfululizo na sita kwa jumla katika kipindi cha miaka saba.
Hakuwahi kupoteza mechi nne mfululizo tangu aanze ukocha mwaka 2008 kabla ya vipigo kutoka kwa Tottenham Hotspur 2-1 kwenye Carabao Cup (Oktoba 30), Bournemouth 2-1 (Novemba 2) na Brighton 2-1 (Novemba 9) ligini na Sporting Lisbon 4-1 katika Klabu Bingwa Ulaya (Novemba 5).
Guardiola hakuwa ameonja kichapo katika michuano 32 ya ligi kabla ya kujipata pabaya dhidi ya Bournemouth.
“Mafanikio yetu si ya milele. Baada ya miaka saba hapa na mataji sita ya Ligi Kuu, huenda timu nyingine inastahili taji,” akasema Guardiola, 53, ambaye vijana wake wako pointi tano nyuma ya viongozi Liverpool.
Kambini mwa City, Guardiola ametimiza malengo ya waajiri kutoka Milki za Kiarabu kwa kushinda kila kitu; Ligi Kuu (mara sita), Kombe la FA (tatu), Kombe la Carabao (nne), Klabu Bingwa Ulaya (moja), Kombe la Ngao (mbili), Klabu Bingwa Duniani (moja) na Uefa Super Cup (moja).
Hajaamua kama anataka kuendelea kuwa ugani Etihad, ingawa kandarasi yake na City inayokatika mwisho wa msimu huu inamruhusu kuitisha nyongeza ya mwaka mmoja.
Kama kawaida yake, Guardiola huenda kuzungumza na mabwanyenye hao Waarabu mwisho wa msimu, lakini majuzi ameonyesha hatafanya hivyo.
Guardiola, ambaye ni kocha analipwa mshahara wa juu duniani katika soka (Pauni 20 milioni kila mwaka), amekuwa akilia kuwa majeraha yamevuruga mipango ya City msimu huu.
Kabla ya kujitosa katika ukocha mwaka 2007, baba huyo wa watoto watatu alikuwa kiungo mkabaji katika klabu za Barcelona, Brescia, Roma, Al Ahli Doha na Dorados.