Soko tayari na moto la nyama za Dorper ‘Majuu’
FRED Memusi, ambaye ni mkazi wa Narok, alilelewa katika familia ya ufugaji.
Akiwa mzaliwa wa maeneo kame (ASAL), Memusi aliishia kufuata nyayo za wazazi na mababu zake.
Kwa mantiki hiyo, kurithi kizazi hicho cha ufugaji kwa Bw Memusi lilikuwa jukumu rahisi ambalo ni sawa na kuutwaa mfumo wa maisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine jinsi wakati unavyosonga.
Kwa sababu hiyo, nyama imekuwa mlo wao wa kawaida karibu kila siku.
Baada ya Memusi kutwaa hatamu kutoka kwa watangulizi wake, alianza kwa kufuga ng’ombe aina ya ‘zebu’ na kisha baadaye kutwaa aina nyingine itambulikayo kama ‘Sahiwal.’
Jinsi siku zilivyosonga, alipanda zaidi, hivyo kumiliki fahali aina ya ‘Brahman’ ambayo asili yake ni ng’ombe wa nyama kutoka Amerika.
Pia, alijitosa kwenye ufugaji wa ng’ombe wa Kiborana, kwa minajili ya nyama.
Akisukumwa sana na wazo la kuhakikisha nchi ina usalama wa kutosha wa mlo wa nyama, Memusi aligundua mbinu nyingine ya ufugaji – kukumbatia kondoo aina ya Dorper.
Hii ni aina mpya ya kondoo ambayo asili yake ni Afrika Kusini na hufugwa kwa minajili ya nyama.
Ni aina iliyoboreshwa kupitia kondoo aina ya Dorset Horn na Balckhead Persian.
Nyama ya kondoo aina ya Dorper inasifika kufuatia utamu wake na nyama yake ikiwa ni laini.
Akiwa mwingi wa tajiriba katika ufugaji kondoo hao wa kisasa, Memusi, ambaye ni mwaanzilishi wa Katakala Farm anakiri kuwa Dorper ni ya kipekee.
Watoto wa Memusi wamekuwa wapenzi wakuu wa nyama ya Dorper.
“Wanangu huishi mijini na huwa nafuatilia sana wanachokula. Kila wakati wanapokuwa likizo na wanapotembea mashambani, nyama ya kondoo aina ya Dorper ndiyo chaguo lao kuu,” akasema Memusi kwenye mahojiano na Taifa Dijitali.
Kulingana na mfugaji huyo, katika kipindi cha likizo Dorper kadhaa huishia kuchinjwa ili kukidhi mapenzi yao kwa nyama hiyo.
“Nyama ya kondoo ndiyo kipenzi chao. Awali, hawangeweza kutofautisha kati ya nyama ya kondoo aina ya Dorper na wale wa kawaida. Hata hivyo, jinsi siku zilivyosonga wamejua kutambua tofauti iliyoko,” akaelezea.
Tofauti na ya wanyama wengine, nyama ya Dorper ni nyororo mafuta yake yakisambazika kila mahali kwenye nyama.
Hali hiyo imeipa nyama hiyo utamu wa kipekee, hivyo kuifanya kutamanika na wengi.
Kufuatia maradhi yanayohusishwa na lishe, watu sasa wameanza kuwa makini kuhusu siha.
Kauli ya Memusi inaungwa mkono na mfugaji mwingine wa Dorper, Sheilla Koech kutoka Kaunti ya Baringo.
Akiwa kwenye ufugaji huo kwa muda wa miezi sita sasa, anasema watoto wake pia hupenda kula nyama za Dorper.
“Nyama za Dorper ni chaguo lao la kwanza. Haziwasababishii athari zozote za kiafya kama watoto ambao mara nyingi lazima kuwe na umakinifu katika ulaji wa nyama,” Sheilla anasema.
Cha kuridhisha zaidi kulingana na Memusi ni kwamba wapenzi wa nyama ya kuchoma (choma) hawahitajiki kuongeza chumvi kwenye nyama ya Dorper kwani tayari huwa na chumvi yake asilia.
Dorper ni rahisi kukuza, hivyo kwa wafugaji wanoendeleza ufugaji eneo tambarare kwa sababu huchangamkia malisho ambayo mengine yanawafaa kimatibabu.
Dorper inazingatiwa kuwa muhimu, hivyo kwa wanaofuga kondoo hao kwa minajili ya biashara ya kuuza nje ya nchi wanafaidi pakubwa.
Safari ya Memusi katika ufugaji wa Dorper ilianza mwaka 2019 kwa kondoo 20 pekee wa kike.
Leo hii, anachezea kondoo wasiopungua 200.
“Niliwanunua kutoka Kaskazini mwa Kenya, pamoja na kondoo dume kutoka kwa mfugaji tofauti ili kusiwe na uzao wa ndani kwa ndani,” akafichua Memusi wakati wa mahojiano ya kipekee wakati wa kongamano la Amagoh Dorper Stud and Training.
Amagoh, ambalo ni shamba la kufuga kondoo lililoko kwenye barabara ya Kangundo, Kaunti ya Machakos, liliandaa kongamano hilo la kuwapokeza ujuzi wakulima wa kondoo jinsi ya kuendeleza ufugaji.
Kongamano hilo liliandaliwa kati ya Julai 18 na 19 mwaka huu, 2024.
Kaulimbiu ya mafunzo hayo ilikuwa ‘Dorper Excellence: Strategies to Unlock Flock Potential and Maintain Quality Consistency,’ yakiongozwa na Phil Rawlins, mtaalamu na jaji tajika wa kondoo aina ya Dorper nchini Afrika Kusini.
Ni kupitia makongamano kama hayo ambapo Memusi ameweza kuboresha kondoo anaofuga, kwa sasa akiagiza wa kiume kutoka Afrika Kusini.
Mfugaji huyu kwa sasa amejikita sana katika uuzaji wa nyama za Dorper katika masoko ya nje ya nchi, hasa akishirikiana wadau wanaotambulika kwa uuzaji bidhaa za kilimo na ufugaji nje ya nchi pamoja na mashirika ya ndege.
Aidha, soko analolenga ni mataifa yauungano wa Waarabu (GCC).
Mataifa hayo sita ya Kiarabu ni pamoja na Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia na Milki za Kiarabu (UAE).
Ikumbukwe kuwa kondoo wa kike huchukua takriban siku 150 (miezi mitano) kuzaa na Memusi anataja kwamba wateja wake wengi hupendelea kondoo wadogo kwa ajili ya nyama wanazouza ng’ambo.
“Licha ya kwamba chaguo hubadilikabadilika, baadhi ya wanunuzi hupendelea kondoo wachanga – wa kati ya miezi minne na sita. Jinsi kondoo alivyo mchanga ndivyo nyama yake ilivyo nyororo na laini, hivyo kuteka bei ya juu,” anaeleza.
Alipoulizwa ni jinsi gani anafaulu kukidhi hitaji kubwa la nyama za kondoo wa Dorper, mfugaji huyo alisema alizindua programu ambapo yeye hutafuta aina hiyo ya kondoo kutoka kwa wafugaji wenza.
“Punde ninapopokea wanyama hao, tunawakagua kujua iwapo wana maradhi, tunawapa chanjo, kuwaweka katika karantini na kuwalisha kwa miezi miwili hadi kufikia uzito unaohitajika,” alifafanua.
Alisema kwa sasa ameweza kuuza zaidi ya Dorper 30,000 ng’ambo, hatua ambayo imemwezesha Memusi kujipanga kihela kila mwaka.
Kondoo wake huchinjiwa kwenye Halal, ili kuhakikisha nyama zinaafikia ubora unaohitajika wa masoko husika.
Kwa sasa yuko kwenye harakati za kubuni mpango wa kushirikisha wafugaji wenye azma sawa na yake ili kumsambazia Dorper.
Kondoo hao ni rahisi kutambua kupitia rangi yao wakiwa wenye mwili mweupe na kichwa cheusi, huku wengine wakiwa weupe mwili wote.
Mtaalam wa Dorper Phil Rawlins, anasifu aina hiyo ya kondoo kutokana na kukua kwake kwa haraka.
“Wanastahimili ukame, ikiwa ni pamoja na kuwa na kiwango cha juu cha nyama,” anasema Rawlins.
Hulka nyingine ya kondoo hao ni uwezo wa mama kulea wanawake vyema.
Kondoo aliyetunzwa vyema wa kati ya miezi mitatu na minne, anaweza kuwa na uzito wa kati ya kilo 15 na 25.
Kulingana na takwimu kutoka kwa Wizara ya Kilimo na Ufugaji, idadi ya kondoo nchini kufikia 2023 iligonga jumla ya 23.2 milioni.
Ripoti hiyo inadokeza, 2023 sekta ndogo ya kondoo ilizalisha Tani Metri (MT) 51,691, thamani yake ikikadiriwa kuwa kima cha Sh34.2 bilioni.
Imetafsiriwa na Kalume Kazungu