Sonko agutuka alijivua mamlaka akabaki uchi
Na BENSON MATHEKA
GAVANA Mike Sonko alipotia sahihi stakabadhi za kuhamisha majukumu muhimu katika serikali ya kaunti ya Nairobi hadi serikali ya kitaifa, alifikiria (kimakosa), kwamba, alikuwa akijiokoa asitumuliwe kama gavana wa kaunti hiyo.
Wengi walimlaumu kwa kukabidhi serikali ya kitaifa majukumu yake, hatua ambayo ingemfanya gavana asiye na ushawishi.
Ilikuwa ni wakati madiwani walikuwa wametisha kumwondoa mamlakani na kulingana na wadadisi, njia ya pekee ya kujiokoa ilikuwa ni kukubali kuhamisha majukumu hayo kwa serikali ya kitaifa ili Rais Kenyatta amsaidie asitumuliwe na akafaulu.
Kile hakufahamu ni yaliyomsubiri baada ya kuhamisha majukumu hayo kwa serikali ya kitaifa.
“Sonko alidhani kwa sababu Uhuru aliwarai madiwani wasimtimue, alikuwa ameshinda. Hakufahamu jinamizi lilikuwa likimsubiri hadi wiki hii alipobaini kwamba, alikuwa amesalimisha mamlaka yake kabisa wafanyakazi wa kaunti walipohamishiwa Shirika la Huduma la jiji la Nairobi (NMS),” asema mdadisi wa siasa Nicholas Mutungi.
Juhudi za Bw Sonko kupinga hatua hiyo ziligonga mwamba na duru zinasema juhudi za kuwasiliana na ikulu kupata maelezo zaidi hazikufua dafu.
Rais Kenyatta alibuni NMS na kuikabidhi mamlaka ya kusimamia huduma muhimu katika jiji la Nairobi na kupigana na mitandao ya wafisadi. “Sonko hakugutuka rais alipolaumu ufisadi kwa kusambaratika kwa huduma jijini Nairobi.
Kilichokuwa kikitawala akili yake wakati huo ni kuokolewa asitumuliwe. Alisahau kwamba, Rais Kenyatta alikuwa akitumia ripoti za ujasusi ambazo zilimtaja (Sonko) kama mshukiwa mkuu katika ufisadi jijini,” alisema Bw Mutungi, ambaye ni diwani wa zamani jijini.
Sonko, ambaye ana kesi ya ufisadi, iliyomfanya apigwe marufuku kukanyaga afisi yake alitetea hatua yake akisema, ilikuwa sehemu ya mpango wa kustawisha jiji la Nairobi na kuimarisha huduma. Alisema aliamua kutafuta usaidizi kutoka serikali ya kitaifa baada ya kuzuiliwa kukanyaga afisini na kukosa naibu gavana.
Kulingana na Sonko, hakulazimishwa kuhamisha majukumu muhimu katika serikali ya kaunti ya Nairobi hadi serikali ya kitaifa
“Ninataka wakazi wa Nairobi waendelee kupata huduma. Ninakabiliwa na kesi ya ufisadi na kwa sababu hakuna Naibu Gavana, hatukutaka mitandao ya wafisadi iendelee kupora pesa za kaunti,” Bw Sonko alisema.
Alisema ni Rais Uhuru Kenyatta pekee ambaye angemsaidia kutekeleza majukumu yake, hatua ambayo wadadisi wanasema ilikuwa makosa makubwa. “Sidhani kwamba ilikuwa hiari ya Sonko kupeana majukumu hayo, alidanganywa naye akadanganyika kuwa, kwa kuepushwa kuvuliwa wadhifa wake, mambo yangekuwa kawaida,” asema Bw Mutungi.
Anasema hali ilimbadilikia Sonko Rais Kenyatta alipobuni NMS na kuikabidhi mamlaka ya kusimamia jiji na kusambaratisha mitandao ya wafisadi katika kaunti ya Nairobi.
“Sonko alisahau kwamba, ni mmoja wa washukiwa wa ufisadi wanaodaiwa kupora mamilioni ya pesa na kubuniwa kwa NMS kulimgeuza gavana kwa jina tu.
Alibaini haya serikali ya kitaifa ilipoteua maafisa 32 wakuu kusimamia huduma muhimu jjjini na kisha wafanyakazi wa jiji wakahamishiwa shirika hilo linalosimamiwa na Muhammad Badi,” alisema mdadisi wa siasa, Jimmy Nyamu.
Bw Badi alimlaumu Sonko kwa kuhujumu NMS na kumtaka kutuliza boli akisema alitia sahihi stakabadhi za kuhamisha huduma za serikali ya kaunti na hafai kulalamika. Kulingana na Nyamu, kuteuliwa kwa maafisa hao kulinuiwa kumkata mikono Sonko ambaye alikuwa ameweka watu wake kusimamia idara muhimu.
“Kuteuliwa kwa maafisa hao kulimfanya Sonko kugundua kwamba, alikuwa amebanwa kabisa na akabaini kuwa stakabadhi alizotia sahihi Ikulu kuhamisha majukumu hazikuwa karatasi za kawaida,” alisema Nyamu.
Wiki jana, Sonko alijaribu kuwazuia wafanyakazi zaidi ya 6,000 wa serikali ya kaunti kujiunga na NMS lakini akapigwa kumbo walipomkaidi. Na siku moja baadaye, kundi lake la Sonko Rescue Team ambalo alikuwa akitumia kutoa huduma jijini Nairobi lilipigwa marufuku kuhudumu jijini.
Wadadisi wanasema Sonko alijikaanga mwenyewe na ingawa kwa sasa juhudi za kumbandua mamlakani zimesitishwa, hana usemi wowote kuhusu shughuli katika kaunti ya Nairobi. “Ametengwa kabisa kuhusu shughuli katika kaunti ya Nairobi.
Zinaendeshwa na NMS na bunge la kaunti, Sonko ni kama shabiki tu,” asema Bw Nyamu. Bunge la kaunti limekuwa likiidhinisha NMS kutumia pesa kwa huduma jijini bila kumhusisha Bw Sonko..
Aidha, kuhamishwa kwa wafanyakazi hao kulihusisha Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) badala ya bodi ya huduma ya umma ya kaunti ambayo wanachama ni vibaraka wa Sonko. Wadadisi wanasema Sonko anafaa kukubali kwamba jiji la Nairobi lina jogoo wapya wanaowika.
“Anachokataa kuamini ni kuwa, maafisa wa serikali ya kitaifa aliokuwa akilaumu kwa kuhujumu serikali yake ndio waliongooza mpango wa kumzima,” asema.
Kabla ya kushtakiwa kwa ufisadi, Bw Sonko alikuwa akilaumu baadhi ya maafisa wa ikulu na afisi ya rais kwa kuhujumu utendakazi wa serikali yake ili kulinda mitandao ya ufisadi.