Suluhu ya Masengeli iko katika korti aliyoidharau lakini akienda anapigwa na butwaa
JUHUDI za dakika za mwisho za mfungwa Gilbert Masengeli kujinusuru asifungwe gerezani ziligonga mwamba jana baada ya ombi lake la kutaka kujiwasilisha katika Mahakama Kuu kukataliwa.
Kufuatia kuhukumiwa kwa kudharau korti mnamo Septemba 13, Bw Masengeli alipewa muda wa siku saba kufika mbele ya Jaji Lawrence Mugambi ili kuondoa hatia ya kudharau korti na kuomba msamaha.
Bw Masengeli hakufanya hivyo. Hata hivyo Alhamisi, saa chache kabla ya makataa ya siku saba aliyopatiwa na Jaji Mugambi kukamilika, Bw Masengeli, kupitia kwa wakili Cecil Miller, alienda kwa Jaji wa Mahakama Kuu Chacha Mwita akitaka amri ya kumshurutisha Jaji Mugambi akubali kumsikiza.
Baada ya siku hizo saba, Bw Masengeli anapaswa kujiwasilisha kwa Kamishana wa Magereza kuanza kifungo chake cha miezi sita.
Bw Miller alimweleza Hakimu Mwita kwamba, hatimaye Bw Masengeli alikuwa tayari kufika kortini ili kutoa maelezo kuhusu waliko wanaume watatu waliotekwa nyara huko Mlolongo na Kitengela mnamo Agosti na ambao kufikia sasa hawajulikani waliko.
“Masengeli yuko tayari kufika kortini leo (Alhamisi) kati ya sita na tisa na nusu alasiri ili kuondoa hatia ya kudharau korti,” Bw Miller alimweleza Jaji Mwita.
Wakili huyo aliomba mahakama imruhusu Naibu Inspekta Jenerali wa polisi wa Utawala kufika katika kikao cha wazi kwa sababu alikuwa na stakabadhi alizotaka kuwasilisha mahakamani.
Hata hivyo, maombi yake hayakuzaa matunda baada ya Jaji Mwita kumweleza kuwa, hangeweza kuagiza jaji aliyemhukumu kuitisha kikao cha kumsikiliza Bw Masengeli.
‘Siwezi kuelekeza jaji mwenzangu (Mugambi) kuacha kesi inayosikilizwa na majaji watatu kushughulikia kesi ya Masengeli,’ Jaji Mwita alisema.
Jaji huyo alisema kuwa, lengo la kutajwa kwa kesi iliyokuwa mbele yake lilikuwa ni kutoa mwelekeo wa kusikilizwa kwa kesi hiyo kwa vile Jaji Mugambi alikuwa akihusika katika kesi nyingine inayowahusu majaji watatu.
Hata baada ya Jaji kusema hayo, Bw Miller aliomba kwa mara nyingine mahakama kusikiza kesi hiyo kwa niaba ya Jaji Mugambi bila mafanikio.
‘Tuko tayari kufika mbele ya jaji wakati wa chakula cha mchana au hata saa tisa na nusu alasiri mahakama itakapoahirisha kesi inayoishughulikia kwa kuwa hukumu ya Masengeli itaanza kutekelezwa leo (Ijumaa) usiku wa manane,’ Miller alisema.
Ombi lake lilipingwa na wakili wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Nelson Havi, akishirikiana na mawakili Levi Munyeri, Hosea Manwa, Eric Theuri na Faith Odhiambo, walioitaka mahakama kutaja kesi hiyo Alhamisi wiki ijayo.
Bw Havi aliambia mahakama kwamba, LSK iliwasilisha ombi lingine la kutaka Jaji Mkuu Martha Koome ateue majaji watatu kusikiliza kesi ya Bw Masengeli kwa vile ni muhimu kwa umma.
‘Mheshimiwa, naomba mahakama hii ipeleke kesi hiyo wa Jaji Mkuu ili ishughulikiwe na majaji watatu. Kesi hiyo itajwe Alhamisi wiki ijayo kwa kuwa ninahudhuria mazishi ya nyanya yangu,’ Bw Havi alimweleza Jaji Mwita.
Lakini Miller alisema kuwa suala lililopo ni kati ya Bw Masengeli na mahakama.
Jaji aliingilia kati na kuagiza kesi hiyo itajwa mbele ya Jaji Mugambi Alhamisi kwa mwelekeo zaidi.Jaji Mwita alitoa maagizo hayo huku Jaji Mkuu Martha Koome akimuapisha Douglas Kanja kuwa Inspekta Jenerali wa polisi baada yake kuteuliwa na kuapishwa katika Mahakama ya Juu kwenye hafla ambayo Masengeli alihudhuria.
Adhabu ya Bw Masengeli na kupatikana na hatia ilitokana na kuendelea kupuuza maagizo ya mahakama mara saba.