TAHARIRI: #HarambeeStars isipuuzwe tena
Na MHARIRI
KWANZA ni pongezi wa timu ya taifa Harambee Stars kwa ushindi mkubwa dhidi ya Ethiopia katika uwanja wa kimataifa wa michezo wa Moi, Kasarani Oktoba 14, 2018.
Ushindi huo umeamsha tena ushabiki wa Wakenya katika mchezo wa kandanda, ambao umekuwa ukididimia kila uchao.
Japokuwa mashabiki Jumapili walijazana kwa wingi kutokana na kuwa hakukuwa na ada ya mlangoni, pia ni kweli kwamba walifanya hivyo kutokana na matumaini makubwa waliyo nayo kwa timu yetu ya taifa.
Mara ya mwisho kwa Kenya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ilikuwa mwaka 2004. Tangu wakati huo, tumekuwa tukiondolewa katika hatua za makundi na timu ambazo hazina miundo msingi mizuri kutushinda.
Ushindi wa jana umeiweka Kenya katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa fainali hizo baada ya kusubiri kwa miaka 18. Pia, unatuonyesha mambo kadhaa ambayo kila mdau anapaswa kuyazingatia.
Kutokana na jinsi mashabiki walivyoshangilia, ni wazi kwamba walifurahia kila chenga na kila bao lililofungwa. Kenya tumezoea ushindi katika michezo mingine, hasa riadha. Tumewahi kushinda kikombe katika kriketi, raga, voliboli na hata ndondi. Ni katika mchezo wa mpira wa miguu pekee ambapo hatujakuwa na rekodi nzuri.
Iwapo Harambee Stars itakuwa ikishinda mechi kama ilivyofanya Jumapili, hapana shaka kuwa siku za usoni mashabiki wataanza kuachana na kufuatilia mechi za Uingereza na Uhispania, na kumiminika kwa wingi kila Harambee Stars na vilabu vyetu vitakapocheza.
Kubwa zaidi ni kwa serikali. Ushindi wa jana haukutokana na kujaa kwa mashabiki pekee, bali zile ahadi za kuwatimizia wachezaji maslahi yao. Mchezo wa kandanda ni biashara kubwa ulimwenguni, ambayo inahitaji uwekezaji wa kiwango cha juu.
Serikali inapaswa kuwa na sera maalum ya kuhakikisha kwamba Harambee Stars haitakuwa ikitegemea ufadhili wa wanasiasa na ahadi za kuipa pesa ikifunga magoli.
Ushuru uliopitishwa wa kuzitoza kampuni za bahati nasibu wafaa kuwa ukiifadhili Harambee Stars. Hii ni pamoja na mshahara wa mkufunzi, marupurupu ya wachezaji na mazoezi ya kutosha ya kupimana nguvu na timu zilizopiga hatua katika mchezo huu.
Wizara ya Michezo yapaswa kushika usukani na kutoa ufadhili wa moja kwa moja kwa wachezaji, huku ikifuatilia uteuzi wa timu, ili kila kijana aliye na kipawa apewe nafasi ya kuchezea nchi bila ya kuwepo mapendeleo.