Makala

TAHARIRI: Kaunti zizingatie ‘Punguza Mzigo’

July 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

KUKAMILIKA kwa ukaguzi wa saini zilizowasilishwa na mwanasiasa Ekuru Aukot kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), sasa kunafungua ukurasa mpya katika historia ya nchi.

Kulingana na Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati, kampeni ya kutaka kuifanyia marekebisho Katiba inang’oa nanga rasmi kwa kuwa imetimiza masharti yanayohitajika kisheria.

Kampeni hiyo kwa jina ‘Punguza Mizigo’ inapendekeza kurekebisha Katiba ili kuwe na Rais atakayehudumu kwa kipindi kimoja cha miaka saba. Hali hiyo itawaondolea Wakenya mzigo wa kwenda uchaguzini mara mbili kumchagua rais baada ya kila miaka mitano, ikizingatiwa uchaguzi wa urais ndio ghali zaidi.

Vile vile kupitia chama cha Thirdway Alliance, Punguza Mizigo inataka kupunguzwa maeneo bunge kutoka 290 hadi 94 pekee.

Kati ya mambo ambayo Punguza Mzigo unataka viti vya Wabunge Maalum na madiwani maalumu viondolewe, sawa na vya Wabunge Wawakilishi wa Wanawake 47.

Punguza Mzigo inapendekeza Serikali za kaunti zitengewe asilimia 35 ya Mapato ya Kitaifa wala sio asilimia 15 ilivyo katika katiba ya sasa, na mshahara wa Rais usizidi Sh500,000 kila mwezi na ule wa wabunge usizidi Sh300,000 kwa mwezi.

Kama kawaida ya Kenya, huenda wanasiasa wakaanza kuupinga au hata kufadhili baadhi ya MCAs waupinge mswada huo. Ni msimamo wetu kwamba, japokuwa hatujaona mapendekezo yaliyo kwenye jopo la BBI, tunaamini kuwa baadhi ya yanayopendekezwa na Mswada huu ni mazuri.

Kikubwa hasa ni kupeleka maendeleo mashinani kwa kuongeza kiwango cha pesa kwa kaunti. Wapo wanasiasa watakaodai kuwa pesa hufunjwa katika kaunti, lakini litakuwa jukumu la wananchi na maseneta wao kukaa macho na kuzuia ufujaji huo.

Katiba inasema kuwa iwapo kaunti zozote 24 kati ya 47 zitaidhinisha mswada huo, utakuwa umepita na Bunge la Taifa na Seneti yatajadili kabla ya kwenda kwa Rais aidhinishe ili wananchi wapige kura.

Kila mwananchi angependa Katiba ikirekebishwa imnufaishe yeye kama mtu binafsi, lakini kupitia mswada wa ‘Punguza Mzigo’ kuna uwezekano kwa nchi hii kupiga hatua kubwa kimaendeleo. Hii ni kwa sababu, kwanza kutakuwa na wabunge wachache wa kulipwa mishahara. Pia, pesa zitakazookolewa zitakuwa zikipelekwa katika kaunti, ili ziendeleze maendeleo ambayo sasa hivi yamekwama.