Makala

TAHARIRI: KEBS na ACA zimeshindwa kukabiliana na bidhaa feki?

March 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

TANGU mvua ya msimu ilipoanza kunyesha wiki mbili zilizopita, mijengo kadhaa imeporomoka Kiambu, Nairobi na Mombasa. Sababu kuu ya kuporomoka kwa mijengo hii ni utumizi wa vifaa duni vya ujenzi.

Katika taarifa ya kina tuliyochapisha majuzi, utumizi wa bidhaa ghushi ulitajwa na wataalamu kama sababu kuu ya mijengo kuporomoka.

Mbali na mijengo tuliangazia pia athari kwa afya ya binadamu kutokana na utumizi wa bidhaa ghushi, ambazo kwa kawaida huwa zimetengenezwa kwa tekinolojia duni, kemikali hatari na hazijafikia viwango vinavyokubalika.

Kulingana na wataalamu, biashara hii inaendelea kuimarika kila uchao na inaendelezwa na wafanya biashara ambao nia yao pekee ni utajiri wa haraka.

Na kweli wengi wao wamekuwa mamilionea katika muda mfupi, lakini madhara ya biashara yao yamekuwa ni maelfu kupata magonjwa hatari yasiyo na tiba, vifo, hasara ya ajali na mijengo kuporomoka na kiwango cha ushuru kushuka.

Kinachosikitisha ni kuwa kuna taasisi ambazo zimepewa jukumu la kukabiliana na biashara feki na kuhakikisha bidhaa zinazowekwa sokoni zinafikia viwango vya ubora uliowekwa.

Lakini taasisi hizi zimeonekana kulemewa na kazi ama zinafungia macho watengenezaji na wauzaji wa bidhaa feki.

Imekuwaje kwa watengenezaji bidhaa hizi feki kuzipenyeza hata katika maduka ya rejereja bila taasisi husika kama vile KEBS na Anti Counterfeit Agency (ACA) kufahamu ama kuchukua hatua zifaazo?

Ni makosa ya uhalifu kwa waliopewa jukumu la kuhakikisha Wakenya wanatumia bidhaa za ubora wa juu kukosa kufanya hivyo, kwani hatua hii inaweka maisha ya taifa lote katika hatari kubwa.

Wasimamizi wakuu wa mashirika husika wanapasa kung’atuka ama waondolewe katika nyadhifa zao kwa kuhatarisha maisha ya Wakenya milioni 45 kwa kukosa kufanya kazi yao kikamilifu.

Huenda wakuu hawa wakadai hawana uwezo wa kukabiliana na wahalifu wanaotengeneza na kuuzia Wakenya bidhaa ghushi.

Lakini hatua mwafaka kwa afisa yeyote ambaye anajali hata maisha yake mwenyewe na ya familia yake ni kusema wazi ameshindwa kutokana na sababu hii ama ile.

Makundi ya kutetea watumiaji bidhaa pia yana jukumu kubwa la kuendeleza kampeni ya kitaifa ya kupigana na bidhaa hizi na kuhamasisha kuhusu hatari zake.

Kwa ujumla wajibu wa kukabiliana na bidhaa feki ni wa kila mmoja.