Makala

TAHARIRI: Kisa cha Sharon na Melon kiwe funzo

June 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA MHARIRI

Kuthibitishwa kuwa wasichana Sharon Mitekwa na Melon Lutenyo ni mapacha halisi, kumeibua maswali mengi kuhusu usalama wa watoto wanaozaliwa hospitalini humu nchini.

Wawili hao walitenganishwa katika hali tatanishi miaka 19 iliyopita, walipozaliwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kakamega.

Na kama si uwepo wa mitandao ya kijamii kama Facebook, pengine wangeishi daima wakiwa wametengana.

Ni tukio ambalo limezua midahalo na hisia mbalimbali nchini, tangu Aprili, masaibu yao yalipoangaziwa.

Hata hivyo, funzo kuu na maswali yanayopaswa kuzingatiwa na wadau wote ni ikiwa viwango vya usalama vinavyotolewa kwa wanawake wanaojifungua watoto wao vinafaa.

Kwa muda mrefu, kumekuwapo malalamishi ya mamia hasa miongoni mwa wanawake wanaodai kubadilishiwa watoto au kupokonywa wanapojifungua.

Katika baadhi ya visa, wengine hudanganywa na wauguzi kuwa watoto wao wamefariki, ila shinikizo zao za kutaka kuonyeshwa miili ya watoto hao huwa zinagonga mwamba.

Chunguzi nyingi zimebaini kuwa baadhi ya wauguzi huwa wanashirikiana na wanawake kutoka nje ya hospitali husika kushiriki katika biashara ya kuuza watoto.

Imebainika kuwa mitandao ya biashara haramu ya watoto ni mikubwa, lakini asasi za usalama bado hazijafanikiwa kutegua usiri wa biashara hizo. Cha kushangaza ni kuwa, visa hivi havipo tu katika hospitali za umma, lakini vimesambaa hata katika hospitali za kibinafsi.

Imebainika kuwa mbali na hospitali, baadhi ya vituo vya watoto vimekuwa vikitumiwa kuwaficha wale wanaoibwa.

Kwa hayo, kilicho muhimu kwa serikali ni kuimarisha usalama katika hospitali zote zinazotoa huduma za kujifungulia wanawake.

Vilevile, ni lazima wauguzi wanaopatikana wakishiriki katika biashara hiyo wakabiliwe vikali, kwani licha ya kuibuka kwa visa hivyo, hatujaona washukiwa wakuu wakifikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka. Ikumbukwe kuwa uhalisia huu mpya utakuwa mgumu kwa wasichana hao wawili, hasa mwenzao Mevis Imbaya, aliyeishi akimfahamu Sharon kama dadake.

Wasichana hao wanafaa kupewa ushauri nasaha. Ni lazima mikakati iwekwe ili kuhakikisha kuwa kosa kama hilo halitokei tena, na wanaohusika kukabiliwa vikali ili kuwa funzo kwa wengine.