Makala

TAHARIRI: Maagizo ya korti hayafai kupuuzwa

April 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

MADAI ya hivi majuzi ya Waziri wa Usalama wa Ndani Bw Fred Matiang’i kwamba Idara ya Mahakama inafanya kazi na wanaharakati mbalimbali kutatiza utendakazi wa mashirika ya kiserikali yanavunja moyo.

Mkuu wa polisi Bw Boinnet pamoja na Katibu katika Idara ya Uhamiaji walikaidi maagizo yayo hayo ya mahakama na hicho si kielelezo bora kwa taifa, hasa ikizingatiwa kuwa hizo ni baadhi ya nyadhifa muhimu serikalini.

Idara ya Mahakama ni taasisi huru ambayo huwa kama mlezi na mlinzi wa katiba yetu, na inapaswa kuheshimiwa na si tu watu binafsi, bali pia taasisi mbalimbali za serikali.

Hakuna ruhusa kwa yeyote kuhitilafiana na taratibu za mahakama.

Inasikitisha kwamba kuna mazoea ambayo yameanza kushika kasi kwa baadhi ya viongozi wenye nyadhifa kuu serikalini kudharau maagizo ya mahakama na hata kuishutumu pindi jaji au hakimu anapotoa amri ya wao kufika mahakamani.

Ikumbukwe kuwa sheria ni msumeno, hukata mbele na nyuma na tunafaa kukumbatia maagizo yoyote yanayotolewa na mahakama hizo, yawe yanatupendelea au hayatupendelei, kama ilivyobainishwa na Katibu yetu.

Maafisa wa serikali wanapokaidi maagizo ya mahakama, ina maana kuwa wanakwepa uwazi na uwajibikaji uliowaweka ofisini. Mwaka mmoja haujaisha tangu Mahakama Kuu iamue kuhusu kesi ya Urais ambayo mwaniaji wa Muungano wa NASA Raila Odinga alipinga matokeo ya uchaguzi alioshinda Uhuru Kenyatta.

Wananchi wengi waliipongeza mahakama kwa sababu iliinusuru nchi dhidi ya kutumbukia katika machafuko.

Katika uamuzi huo, ilibainika kuwa uchaguzi huo haukufanywa kwa njia huru na haki na ikaagizwa uchaguzi mpya uandaliwe. IEBC iliratibu Oktoba 26, 2017 kama tarehe mpya ya uchaguzi na ukaendeshwa kadiri ilivyoweza na matokeo yakabainishwa.

Viongozi wanapoamua kupuuza maagizo ya mahakama, wanajaribu kutuambia kwamba wepo raia walio Wakenya zaidi kuliko Wakenya wengineo.

Ni muhimu kufahamu kwamba hakuna yeyote aliye juu ya sheria na kwamba mahakama ni mpatanishi mkuu ambaye kazi yake ni kuhakikisha kwamba haki za kila Mkenya zinalindwa na vyombo vyote vya kisheria.