TAHARIRI: Maandalizi ya mapema yatazaa matunda Stars
Na MHARIRI
MIEZI ya Juni na Julai 2019 itakuwa ya shughuli tele za kispoti kwa timu ya taifa ya soka Harambee Stars.
Kikosi hiki kinachonolewa kwa sasa na mkufunzi Sebastien Migne kimefuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON), kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 15.
Stars watakaoshuka leo dimbani kuvaana na Ghana katika marudiano ya Kundi F jijini Accra walicheza fainali hizi kwa mara ya mwisho 2004 nchini Tunisia. Wakati huo, walikuwa wakiongozwa na kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee.
Kufuzu kwa Stars kuwania ufalme wa Afrika katika jukwaa la soka mwaka huu ni mafanikio ambayo Wakenya wengi waliyatamani kwa muda mrefu ila yakawa hayatimiliki.
Lakini hatimaye wamepata tabasamu baada ya timu hiyo kufuzu pamoja na Ghana kutoka Kundi F.
Zipo ahadi zilizotolewa kama njia ya kuwatia hamasa wanasoka wa Stars ambao kwa kweli walitaabika sana kutua nchini Ghana mnamo Alhamisi wiki hii.
Mojawapo ya ahadi hizo ni ile ya Naibu Rais William Ruto na Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko walipoahidi timu hiyo mamilioni ya pesa iwapo wangeshinda Ethiopia pamoja na kufuzu kwa fainali za AFCON.
Gavana Sonko alitimiza ahadi yake jinsi alivyoahidi na kuwakabidhi vijana wa nyumbani kima cha Sh3 milioni.
Ahadi ya Naibu Rais ya Sh50 milioni ndiyo bado inasubiriwa hasa wakati huu kikosi cha Stars kinapojizatiti kuelekea Ufaransa kujinoa zaidi.
Hizi ni hela ambazo zikitolewa, zitawatia wachezaji na benchi nzima ya kiufundi motisha wanaohitaji zaidi nchini Misri wakati wa fainali kati ya Juni na Julai.
Hata hivyo, kuna haja ya kuwa na hazina thabiti ya timu hiyo ya taifa inapojitayarisha kushiriki kinyang’anyiro hicho cha bara la Afrika.
Kwa sababu ya maandalizi kabambe na ya kufana, itakuwa vyema kwa Serikali, kupitia Wizara ya Michezo kuitengea timu hii bajeti kubwa kuliko ilivyokuwa imepanga kwani timu itahitaji fedha nyingi za maandalizi nchini Ufaransa na hata kufanikisha kampeni zao nchini Misri.
Kwa sababu hiyo, ni wito wetu kuwa Serikali, kwa ushirikiano na mashirika ya kibiashara, inafaa kubuni mikakati ya mapema itakayohakikisha timu hiyo imefanikiwa kupiga hatua katika fainali hizo kutokana hasa na ufadhili mzuri, tena kwa wakati ufaao.
Kocha naye alipwe mshahara na marupurupu yake mapema.
Hali ni hivyo pia kwa vikosi vya kitaifa vya raga na yamkini katika michezo mingineyo kama vile voliboli na riadha.