Makala

TAHARIRI: Matiang'i akabiliane na wahalifu hatari

November 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

SUALA la usalama limekuwa tete mno miongoni mwa Wakenya. Ingawa tuna maafisa wa kutosha wa polisi pamoja na kamati za Nyumba Kumi, imekuwa vigumu mno kwa mtu kujihakikishia kuwa anaweza kuendeleza shughuli zake bila ya kuhangaishwa au kuvamiwa na wakora.

Magenge ya watu yameshuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi. Kaunti ya Mombasa ndiyo ambayo imekuwa ikiongoza kwa visa vya makundi ya vijana. Kumekuwa na makundi kama vile Wakali Kwanza, Wakali Wao miongoni mwa mengine.

Sasa hivi katika kaunti za Murang’a na Nyeri kumejitokeza kundi la Mungiki, ambalo lilikaribia kuangamizwa mwaka 2008 na aliyekuwa Waziri wa Usalama, Marehemu John Michuki.

Katika kaunti ya Nairobi, kumejitokeza genge hatari la Gaza Boys linalohangaisha wakazi wa mtaa wa Kayole. Wafuasi wengi wa genge hilo wameuawa katika muda wa miaka miwili iliyopita, lakini wakazi wa Kayole wanalalamika kwamba genge limeundwa upya na linazidi kuwahangaisha.

Makundi haya ya wahalifu yanatekeleza mauaji na kuwadunga watu visu mchana peupe, huku polisi wakiwa hawawatii mbaroni. Katika maeneo mengi ambako polisi wamejaribu, wamekuwa wakiwapiga risasi na kuwaua washukiwa hao.

Ingawa mashirika ya kutetea haki za binadamu wamekuwa wakilalama kuwa polisi wanaendeleza mauaji ya kiholela, ipo haja kwa wadau wote kupima kati ya haki za binadamu na usalama wa wananchi.

Huenda pengine polisi hawatumii mbinu muafaka za kukabiliana na wafuasi wa makundi hayo, lakini cha msingi ni kwamba ni lazima yakabiliwe vilivyo na kuwahakikishia wananchi usalama wao.

Kwa bahati nzuri wizara ya Usalama wa Ndani inasimamiwa na Dkt Fred Matiang’i. Waziri huyu ameonyesha ulimwengu mzima kwamba anaweza kusimamia masuala yanayomhusu bila ya kurejea nyuma.

Msimamo wake thabiti ambao Wakenya wengi wanauunga mkono, umedhihirika alipokuwa waziri wa Elimu na sasa katika wizara ya Usalama.

Dkt Matiang’i ana jukumu la kupiga msasa jinsi ambavyo masuala ya usalama yanashughulikiwa na maafisa wa polisi. Kuna uwezekano kuwa baadhi ya wakuu wa polisi wananufaika na mali yanayoporwa na wahalifu, pindi wanapowaua wananchi wasio na hatia.

Anapaswa achunguze kwa makini na kuchukua hatua zitakazosaidia kumaliza visa vya magenge. Hata bila ya kuwaua, bila shaka maafisa wa usalama walipata mafunzo ya kukabili watu kama hao.