TAHARIRI: Matokeo mazuri si shule tu bali pia juhudi
NA MHARIRI
Juma lililopita zaidi ya wanafunzi milioni moja waliteuliwa shule watakazojiunga nazo kuanzia mwezi ujao. Kati yao, wanafunzi 31,000 watajiunga na shule za upili za ngazi ya kitaifa huku wengine waliosalia wakijiunga na ama shule za kiwango cha kaunti au kaunti-ndogo.
Hata hivyo, paliibuka vilio miongoni mwa wanafunzi hao waliopita vizuri kwa kupata angaa alama 400, pale walipobaini kwamba shule walizopewa, japo ni za kitaifa, hazijulikani.
Mmoja wa wanafunzi waliosumbuliwa sana na uteuzi huo ni Telvin Gichuki aliyetarajia kujiunga na shule maarufu ya kitaifa, Alliance Boys High, lakini akagutushwa alipopewa Shule ya Upili ya Kabianga. Mwanafunzi huyo anayetoka Kaunti ya Embu alizoa jumla ya alama 434 katika mtihani wa kitaifa wa KCPE.
Mwingine ni msichana Ruth Chaka anayetoka Kaunti ya Kwale ambaye alikwangura alama 446. Alishangaa pale alipoitwa katika Shule ya Mama Ngina badala ya Alliance Girls High.
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa wanafunzi wengi waliochagua shule za kitaifa waliteua zile maarufu kama vile Alliance, Mang’u, Starehe, Pangani Girls, Kenya High na nyingine kadhaa. Hivyo basi, hawakutarajia kuteuliwa katika shule za kitaifa zilizokwezwa hadhi hivi majuzi.
Kwa jumla Kenya ina shule 103 za kitaifa ambapo wakati wa kufanya uteuzi, hizo zote huwekwa kwenye mizani sawa, zote zikichukuliwa kama shule za kitaifa bila kujali ni lini shule hizi zilipokwezwa hadhi.
Kwa hivyo wanafunzi wanafaa waambiwe kuwa si lazima waitwe katika shule maarufu kama vile Alliance au Mang’u na nyinginezo chache ndipo wapite mtihani wao wa kidato cha nne vizuri.
Ifahamike kuwa, japo mazingira ya shule huchangia kwa kiasi fulani kwenye matokeo ya mwanafunzi, matokeo ya mtihani hutegemea hasa bidii na kujitolea kwa mwanafunzi binafsi.
Kadhalika, wanafunzi wanafaa wafahamu kuwa wapo wenzao watakaojiunga na shule za ngazi ya kaunti au hata kaunti-ndogo ambao watakwangura alama za A kwenye KCSE.
Wala wizara ya elimu haifai kulaumiwa kwa sababu Alliance High, kwa mfano, haiwezi kuwabeba wanafunzi wote 31,000 waliofuzu kujiunga na shule za kitaifa. Pili uteuzi huo hufanywa kwa njia ya auto, kumaanisha kuwa hamna mwanadamu anayehusika katika kumteulia mwanafunzi shule bali shughuli hiyo hufanywa na kompyuta.