Makala

TAHARIRI: Muafaka usiwe kifo cha upinzani

March 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

MALUMBANO ndani ya vyama tanzu vya upinzani unaendelea kupandisha joto la kisiasa ambalo lilikuwa limezimwa na mkutano wa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga.

Jumanne, Seneta wa Bungoma Moses Wetangula alivuliwa wadhifa wake wa kiongozi wa wachache bungeni hatua ambayo ilivikera sana vyama vya Wiper, ANC na Ford Kenya.

Chama cha ODM kilimfurusha Bw Wetangula licha ya vinara wa NASA, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Wetangula na Bw Odinga kutoa maagizo ya kukomesha hatua hiyo.

Japo vyama vya kisiasa vina demokrasia ya kuadhibu wanachama waasi, ni vyema mizozo ya ndani ilisuluhishwe kimya na viongozi bila kuchochea uhasama wa kisiasa haswa miongoni mwa jamii.

Mabadiliko yanayoshuhudiwa NASA katika usimamizi wa bunge yalianza baada ya mkutano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Tungetaka kusisitiza umuhimu wa kuwa na chama cha upinzani bungeni ili kukosoa maovu ya serikali.

Bw Odinga alichukua hatua ya busara sana kuweka kando tofauti zake za kisiasa na kukutana na rais, lakini ni vyema Waziri huyo Mkuu wa zamani awape nafasi viongozi wengine wanaotaka kuendelea kuwa kwa upinzani.

Hatua ya ODM kumtimua Seneta Wetang’ula katika wadhifa huo imechukuliwa na wengi kama usaliti wa kisiasa hatua ambayo huenda ikaanzisha siasa za 2022.

Siasa zina ushindani mkubwa na ingekuwa vyema kutoanzisha mjadala wa uchaguzi wa 2022 ili kutoa nafasi kwa serikali kuu na zile za kuanti kuwahudumia Wakenya kabla ya kuingia katika mchakato mwingine wa kisiasa.

Bw Musyoka na wenzake walimuomba Rais Kenyatta awape sikio na tunasisitiza umuhimu wa kufanyika kwa mdahalo wa viongozi wote.
Japo mkutano wa rais na Bw Odinga umewapa wengi matumaini ya kutuliza joto la kisiasa nchini, ni vyema kutopuuza mchango wa vinara wenza katika upinzani.

Madhumuni ya kuungana kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga yawe kuunganisha Wakenya wote na wala si kuua upinzani ambao mchango wake ni muhimu sana kuhakikisha mali ya umma imelindwa na kutumika ipasavyo.

Bw Odinga anapaswa kujitokeza wazi kuelezea iwapo chama chake kimemezwa na Jubilee ili kutoa nafasi kwa vyama vingine vyenye uwezo wa kuikosoa serikali.