Makala

TAHARIRI: Ni aibu kwa maseneta kuhusishwa na hongo

August 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

KABLA ya kisa kuhusu ufisadi ndani ya Bunge la Kitaifa kufifia, madai mengine ya kutisha yameibuka kuhusiana na Bunge la Seneti.

Wiki moja na nusu hivi tu baada ya wabunge kudaiwa kupokea Sh30, 000 ili kupinga ripoti kuhusu sukari ya sumu, sasa inadaiwa kwamba Bunge la Seneti nalo lilikuwa linadai Sh100 milioni ili kutupa ripoti kuhusu ardhi ya Ruaraka ambako Shule ya Upili ya Ruaraka na ya Masingi ya Drive -Inn zimejengwa.

Ripoti kuhusu sakata ya sukari chafu ilikuwa imependekeza kwamba waziri wa Fedha Henry Rotich, mwenzake wa Afrika Mashariki Adan Mohamed na balozi wa India Willy Bett wachunguwe kuhuisiana na kashfa hiyo ya uingizaji sukari chafu nchini bila kufuata kanuni zilizowekwa.

Kulingana na tetesi, kuna wale viongozi ambao walilenga kuwaepusha maafisa hawa wakuu serikalini balaa hii ya kuchungwa na pengine kushtakiwa endapo wangepatikana na hatia.

Kilichoshangaza ni kwamba Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale na Kiongozi wa Wachache John Mbadi, walionekana kuzungumza kwa sauti moja kupinga ripoti hiyo kuhusu sukari wakati wa mjadala ndani ya Bunge.

Wananchi wengi walitarajia kuona ukweli kuhusu suala hilo lililoonekana kuwa tata likichanganuliwa na kufichuliwa wazi na waliokuwa lawamani kuchunguzwa ili hatimaye hatua ya kisheria ichuliwe dhidi yao ushahidi wa kosa ukipatikana.

Hata hivyo, yaliyotokea yalitamausha Wakenya wengi. Matamanio ya kuupata ukweli yalifikia kikomo.

Mnamo Jumatano, Kamati ya Uhasibu na Hazina ya Umma (PAC) ilijitenga na madai kwamba seneti ilidai Sh100 milioni ili kufunika sakata ya uuzaji wa ardhi ya Ruaraka.

Mwenyekiti wa kamati hiyo alinukuliwa akipinga, madai ya mwenye ardhi hiyo Francis Mburu kwamba, aliwanukuu baadhi ya maseneta wakiitisha hongo katika bunge.

Bw Kajwang’ alisema Bw Mburu alikuwa akiwapotosha Wakenya kwa nia ya kufunika ukweli kuhusu umiliki wa ardhi hiyo iliyokumbwa na mzozo wa uuzaji. Bw Mburu alidai kwamba aliwasilisha nukuu hizo kwa Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI).

Huku vita dhidi ya ufisadi vikizidi kupamba moto huku Rais Uhuru Kenyatta akiwa kwenye usukani, litakuwa jambo la aibu wabunge kwenda kinyume cha haya.

Inashangaza kuona wanaoaminika kuwa watetezi halisi wa Wakenya wakionekana kuwa watetezi wa maslahi yao ya kibinafsi. Mabunge yote yamtendee Mkenya haki kwani jukumu lake kuu ndilo hilo hasa.