TAHARIRI: Nyongeza ya ushuru iwafae Wakenya
NA MHARIRI
MAMLAKA ya Ushuru Nchini (KRA) imetoa mapendekezo mapya yanayolenga kuwatoza Wakenya ushuru zaidi pamoja na kuweka mikakati ambayo itawakazia kamba wale wanaolenga kutafuta mikopo miongoni mwa masuala mengine.
KRA imewasilisha mapendekezo yake kwa bunge la kitaifa ambayo tayari yamewasilishwa kwa Hazina Kuu. Mapendekezo hayo yanalenga kutoza ushuru biashara zinazoendeshwa kidijitali, wanachama wa mashirika ya kitaalam , wachezaji kamare na biashara hasa zinazohusika na utoaji huduma na ambazo huwa hazilipi ushuru.
Wanaokosa kulipa ushuru pia huenda wakaathiriwa na mapendekezo hayo ambayo yanataka kuwa wanyimwe mikopo hadi watimize wajibu huo.
Hii ni kwa sababu wakikosa kulipa ushuru, mapendekezo hayo yakiidhinishwa, wataorodheshwa kwa mashirika yanayoangazia watu wanaokosa kulipa mikopo, na hivyo kuwanyima fursa ya kukopeshwa na mashirika yoyote ya kifedha.
Wakenya wengi hawana pingamizi ya aina yoyote kwa KRA kukusanya ushuru, lakini tatizo kuu ni kwamba wengi wanahisi kuwa pesa hizi hazitumiki jinsi inavyostahili. Ushuru wanaotozwa Wakenya ni mkubwa mno na ndiposa watu wanatarajia kuona hali ikibadilika kwa manufaa yao.
Kila kukicha kuna kashfa mpya ya ufisadi inayochipuka, jambo ambalo linawatamausha wengi wanaotazama stakabadhi zao za mishahara kila mwezi, na kuona kiasi wanacholipia ushuru.
Ni muhimu kwa KRA kufanya kila juhudi kwa kweli kuhakikisha kuwa wote wanaostahili kulipa ushuru wanalipa, na kuhakikisha kuwa pesa hizo zinatumika kwa madhumuni yanayostahili.
Serikali na wahusika wote lazima watambue uzito wanaouhisi Wakenya katika ulipaji ushuru na kuwajibikia vilivyo pesa wanazokusanya.
Rais Uhuru Kenyatta amejitokeza kupiga vita ufisadi, lakini ukweli ni kwamba lazima wote waliopewa majukumu mbalimbali serikalini wawe na nia sawa na hiyo, watu waaminifu na wenye ukweli na wazalendo kuhakikisha kuwa wanapatia taifa hili matumaini ya siku zijazo na vizazi vijavyo.
Bila shaka, Wakenya wakiona faida ya ushuru wao watakuwa tayari kulipa bila manung’uniko. Lakini inakuwa jambo gumu ikiwa wanakosa huduma muhimu, na kupitia mikononi mwa watumishi fisadi kupata huduma wanazolipia kwa kutozwa ushuru.