TAHARIRI: Oparanya aimarishe utendakazi wa kaunti
NA MHARIRI
WAKATI wa Hotuba ya kila mwaka kuhusu hali ya ugatuzi mwaka 2018 Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya alionekana kuelewa kinachotatiza ugatuzi kutekelezwa kikamilifu.
Miezi tisa baadaye, sasa Bw Oparanya amechukua rasmi uongozi wa Baraza la Magavana nchini, baada ya kuwashinda magavana wenzake wanne.
Magavana Profesa Peter Anyang’ Ngong’o (Kisumu), Bi Anne Waiguru (Kirinyaga), Bw Salim Mvurya (Kwale) na Bw Jackson Mandago (Uasin Gishu) pia walikuwa wakimezea mate wadhifa huo.
Ingawa kuna vikwazo kutoka kwa Serikali Kuu, asilimia kubwa ya kukosekana manufaa kamili ya ugatuzi inatokana na uongozi wa kaunti zenyewe.
Kwa mfano, Tume ya Mishahara na Marupurupu ilikuwa imeweka viwango vya pesa ambazo madiwani wanafaa kulipwa. SRC iliagiza kuwa marupurupu ya MCA yasipite Sh80,000. Lakini baadhi ya kaunti ikiwemo Kakamega, zilipuuza sheria hiyo na kuwapa MCA hadi Sh121,026.
Ingawa ni kweli kuwa Hazina Kuu haitumi pesa za kutosha katika kaunti, baada ya magavana na serikali zao wamekuwa wakitumia kiwango kikubwa cha pesa hizo chache katika shughuli zisizohusiana na maendeleo.
Mojawapo ya mambo yanayofaa kupewa umuhimu zaidi na kaunti chini ya uongozi wa Bw Oparanya, ni elimu katika ngazi za sekondari, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu.
Serikali iliongeza muda wa wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza hadi Ijumaa wiki hii. Wanahabari tunaendelea kupokea visa vingi vya watoto werevu walioitwa kujiunga na shule za upili za kitaifa lakini hawana uwezo wa kuendeleza masomo yao.
Katika Baraza la Magavana kuna watu wenye uzoefu mbalimbali. Bw Oparanya anapaswa kuwa kiongozi anayesikiza na kushauriana na wenzake kuhusu njia bora za kuboresha kaunti zote 47, hasa kielimu.
Kuna watu watakaoteta kuwa miundo msingi haishughulikiwi sana, lakini hakuna uwekezaji bora kushinda katika elimu ya watoto.
Baraza la Magavana chini ya Bw Josephat Nanok lilianza kupata nguvu na kutekeleza shughuli zake kwa kujitolea zaidi. Sasa Bw Oparanya na wenzake waliochaguliwa, wanapawa kutumia fursa ya kuwepo masikizano nchini, kuendeleza mfumo wa ugatuzi.
Japokuwa gavana wa Kakamega anatoka upinzani, uongozi wa kaunti unahitaji ushirikiano na serikali kuu. Yafaa wote waliochaguliwa waendeleze ushirikiano huo kwa manufaa ya wananchi.