TAHARIRI: Serikali ijitolee kufaulisha sensa
Na MHARIRI
SHUGHULI ya kuhesabu watu maarufu kama Sensa inatarajiwa kung’oa nanga kote nchini usiku wa Jumamosi, serikali ikilenga kufahamu idadi ya Wakenya ili kuisadia kupanga matumizi ya rasilimali za nchi kwa muda wa miaka 10 ijayo.
Hii itakuwa sensa ya sita nchini tangu uhuru. Sensa za awali zilifanyika miaka ya 1948, 1962, 1969, 1979, 1989, 1999 na 2009.
Itakuwa sensa ya kwanza tangu mfumo wa utawala wa ugatuzi uanze baada ya Katiba Mpya ya mwaka wa 2010.
Tayari serikali imetangaza kila Mkenya lazima ahesabiwe na atakayekosa au kuvuruga shughuli hiyo atapigwa faini ya Sh100,000 au kifungo gerezani.
Wanasiasa nao wiki hii wamekuwa kwenye hekaheka za kurai raia wanaoishi mijini kurejea kwenye kaunti zao za asili ili kuhesabiwa wakisema idadi yao ndiyo itatumika kuamua ugavi wa mapato kutoka kwa serikali kuu.
Hata hivyo, serikali ina kibarua kigumu kuhakikisha kuwa shughuli hiyo inafanikiwa ikizingatiwa raia wengi bado wapo gizani kwa kutojua masuala mengi kuhusu namna itakavyoendeshwa na cha kutarajia.
Kwanza, serikali inafaa kuhakikisha kwamba wahalifu hawatumii Sensa kupora raia nyakati za usiku kwa kujifanya kuwa maafisa wa kuwahesabu watu hasa katika mitaa mbalimbali mijini.
Tunaunga tangazo la Shirika la Takwimu Nchini (KNBS) kwamba maafisa wa Sensa watakuwa na vitambulisho na wataandamana na afisa wa polisi katika kila nyumba.
Pili KNBS ilisema shughuli hiyo itaendeshwa haraka iwezekanavyo kwa njia za kielektoniki kulingana na mali ya kila familia.
Hata hivyo, hilo pekee halitoshi na ni vyema kwa serikali kuongeza maafisa wanaoshika doria usiku huo huku raia pia wakitahadharishwa dhidi ya kurandaranda ili kupunguza visa vya utovu wa usalama.
Serikali pia inafaa kutafakari upya kuhusu amri inayohitaji watu watakaokuwa safarini usiku huo kusimamishwa barabarani ili kuhesabiwa kwanza kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari zao.
Je, wagonjwa walio katika hali mahututi wanaowahiwa hospitalini pia watasimamishwa?
Sensa haifai kuvuruga shughuli za watu na wanaosafiri wanafaa kuruhusiwa kupiga nambari maalumu itakayotolewa au kufika katika afisi za maafisa wa utawala ili idadi yao ijumuishwe na wengine.