TAHARIRI: Siasa za 2022 zikomeshwe
Na MHARIRI
WIKI chache baada ya viongozi kuombana msamaha wakati wa maombi ya kitaifa, cheche za siasa za 2022 zimeibuka tena.
Naibu Rais William Ruto aliongoza kikosi kikubwa cha wanasiasa wa Jubilee katika Kaunti ya Kiambu ambapo siasa za 2022 zilitawala.
Naye kiongozi wa ODM Raila Odinga alikuwa Mombasa ambapo pamoja na Gavana wa eneo hilo Hassan Joho walimshambalia Bw Ruto kwa kampeni za mapema.
Ni makosa makubwa kwa viongozi kuweka nchi katika hali ya uchaguzi kila mara. Hii ni kwa sababu badala ya kutekeleza ahadi ambazo walitoa, fikra za Wakenya zinawekwa mawazo ya uchaguzi usio na kikomo.
Ingawa ni haki ya wanasiasa kujipanga kwani azma yao kuu ni kuwa madarakani, ni jambo la busara zaidi kuafikia haya kwa kujishughulisha zaidi na utendaji kazi unaolenga kuinua maisha ya Wakenya na kuhakikisha demokrasia na utawala bora zinazingatiwa.
Hii tabia ya kujadili siasa za ni nani atakayechaguliwa rais 2022 asubuhi hadi jioni kana kwamba zitaboresha maisha ya Wakenya ni ya kupotosha na iliyopitwa na wakati. Hii ni tabia ya kuelekeza nchi gizani badala ya mwangani.
Siasa ambazo Wakenya wanahitaji kwa sasa ni jinsi ugawaji wa raslimali za kitaifa unavyoweza kufanywa kwa uwazi ili kusaidia kila pembe ya nchi, kumaliza ufisadi, kuboresha elimu, kuzalisha chakula zaidi, uchumi, na mambo mengine yanayohusu ustawi wa nchi.
Siasa za wakati huu pia zinafaa kushirikisha masuala ya sheria zinazostahili kufanyiwa marekebisho ili kumfaa mwananchi.
Wanasiasa wanapasa kufahamu kuwa walichaguliwa kufanyia wananchi kazi wala sio kuwasumbua kwa mijadala isiyo na maana kwao kwani wakati wake haujafika.
Mikakati yao ya 2022 inaweza kuwa na manufaa zaidi iwapo itajengwa kwenye misingi ya yale ambayo watakuwa wamefanyia wananchi kufikia wakati huo.
Wanasiasa wanapasa kukomesha mijadala ya 2022 na badala yake waheshimu wapigaji kura kwa kutekeleza waliyoahidi.
Iwapo kweli Bw Ruto na Bw Odoinga ni viongozi wanaopea maendeleo kipau mbele, wanapaswa kukomesha wanasiasa wanaondamana nao kuhusu siasa za 2022.