Makala

TAHARIRI: TSC na Wizara ya Elimu zimalize tofauti zao

December 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

Mzozo kati ya Wizara ya Elimu na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuhusu alama za kujiunga na vyuo vya ualimu unafaa kusuluhishwa haraka iwezekanayo.

Misimamo mikali kati ya Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia (pichani) na Waziri wa Elimu Amina Mohamed huku kila mmoja akivutia upande wake kutetea uamuzi maoni yake haufai kamwe.

Hatua ya waziri Mohamed kushusha gredi ya kujiunga na vyuo vya ualimu kutoka alama ya C+ hadi C kwa kiwango cha diploma na C hadi D+ kwa kiwango cha vyuo vya shule za msingi imetia wadau wa elimu nchini katika hali ya suitafahamu.

Uamuzi wa Bi Mohamed ulichochewa na hali kuna uhaba mkubwa wa walimu maeneo fulani nchini na pia kiwango cha elimu humo kimedorora mno katika miaka ya hivi karibuni.

Waziri alitaja kuwa mashambulio ya Al Shabaab yamechangia hali hii eneo la Kaskazini mashariki. Maeneo aliyorejelea waziri ni kaunti zifuatazo; Turkana, Samburu, Wajir, Marsabit, Isiolo,Manderra,Garissa, Lamu,Baringo,Narok,Kajiado,Kwale,Kilifi, Taita Taveta,Tana river na Pokot Magharibi.

Bi Mohamed anazidi kuelezea kwamba baadhi ya walimu humo huomba kuhamishwa kutoka maeneo hayo huku wale wanaotumwa humo kukataa kuripoti kwa kuhofia usalama wao. Hii ndio maana waziri anaonelea maeneo haya yanafaa kufunzwa walimu wenyeji waliosomea humo. Kutokana na hali ya kiwango cha chini cha masomo ndipo wizara iliamua kushusha gredi hizo za kuingia vyuoni.

Msimamo wa Wizara ya Elimu umekumbatiwa na Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) kikiongozwa na Wilson Sossion aliyedai kwamba kushusha alama kujiunga na vyuo hivyo haitamaanisha kiwango cha elimu maeneo hayo kitashuka.

Kwa upande wake Afisa Mkuu wa TSC Bi Macharia, anashikilia wale watakaojiunga na taasisi hizo za ualimu bila kuzingatia alama zile zimewekwa hawatapata ajira katika tume hiyo.

Ingawa mzozo huu umeleta utata katika sekta ya elimu kwa ujumla, ni aibu viongozi wanaoaminika kuonekana kutofautiana kuhusu sera za elimu ilhali wao ndio wanaotegemewa kutoa mwongozo rasmi kuhusu ualimu na masuala yote ya elimu kwa ujumla.

Viongozi na wadau hawa wa elimu wanafaa kuketi pamoja na kutatua masuala haya badala ya kuonyesha tofauti zao hadharani kupitia vyombo va habari.