Makala

TAHARIRI: Tujitolee kutenda mema Krismasi

December 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

DESEMBA 25, mamilioni ya Wakenya wamemuika na wenzao kimataifa kusherehekea sikukuu ya Krismasi.

Siku hii ni muhimu katika kalenda ya Wakristo kwani ni ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Hata hivyo, kadri na jinsi miaka inavyosonga, hii ni siku ambayo imezidi kubadilika kwa misingi ya vitendo vinavyofanya kuiadhimisha.

Ijapokuwa kuna maovu ambayo hutokea wakati watu wanapojumuika wakidai ni mbinu zao za kusherehekea, kuna mengi mema ambayo siku hii hutolea nafasi wananchi kutenda.

Huu ndio wakati ambapo wengi wetu hupata nafasi ya kutembelea wenzetu wasiojiweza katika jamii na kuwapelekea misaada ya aina mbalimbali.

Ukarimu huu, ukifanywa kwa moyo wa kujitolea bila nia ya kujitafutia umaarufu, hakika ni hatua ambayo inastahili na inahimizwa kidini.

Mafunzo ya Kikristo pamoja na dini nyinginezo ikiwemo Kiislamu huhimiza waumini kuhusu hitaji la kusaidia watu wasiojiweza katika jamii.

Hili linaweza kutekelezwa kwa njia tofauti ikiwemo kutembelea makao ya watoto mayatima, na kutembelea wagonjwa waliolazwa hospitalini.

Vile vile, kuna watoto wengi ambao walipokea matokeo bora ya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) lakini wanatoka katika familia zilizolemewa kifedha.

Tunaposherehekea, tukumbuke kikundi hiki cha watoto ambao tunaweza kujitolea kuwasaidia ili ifikapo Januari wapate kuendeleza elimu yao ya shule za upili bila matatizo.

Jambo jingine ambalo hushuhudiwa wakati huu ni maafa yanayosababishwa kwa njia mbalimbali ikiwemo ajali za barabarani na unywaji wa pombe haramu au unywaji wa pombe kupita kiasi.

Wakenya wanafaa wakumbuke kuchukua tahadhari kwa kila jambo wanalofanya kwani sherehe haimaanishi tumefika mwisho wa maisha.

Bado kuna majukumu tele yanayotusubiri mwaka ujao, kwa hivyo ni muhimu tujilinde wakati wote.

Wengi hutilia maanani tu hitaji la kujihadhari barabarani wakati wa usafiri, kwani maafa yanayotokea barabarani ndio huangaziwa zaidi.

Lakini, inafaa pia kuwa makini kwa vitendo vyetu ikiwemo vyakula tunavyotumia katika msimu huu.

Huu ndio wakati ambapo utakuta wengi wanasahau umuhimu wa kujilinda afya zao kwa kula vyakula ambavyo si salama kwa afya na vile vile, kubugia pombe bila mpangilio.