Makala

TAHARIRI: Tuongeze juhudi kuangamiza TB

March 26th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

ULIMWENGU ulipoadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani Jumamosi, jambo moja lililojitokeza wazi ni kwamba Wakenya 29,000 walikufa mwaka jana kutokana na ugonjwa huo.

Hata takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) zinaonyesha kuwa TB ni ugonjwa wa pili kwa kuua watu duniani, ambapo 4,500 huaga dunia kila siku.
Ugonjwa huu umekuwa hatari zaidi, kutokana na kuzuka kwa Kifua Kikuu ambacho hakisikii dawa.

Tatizo kubwa linalowakumba Wakenya wengi ni kuwa, hata mtu anapoanza kukohoa mfululizo, huogopa kwenda kumwona daktari kutokana na itikadi isiyokuwa ya ukweli kuwa mtu akiugua TB bila shaka atakuwa ana virusi vya Ukimwi.

Ni kweli kwamba mtu anapokuwa na virusi vya HIV, huwa na kinga dhaifu na maradhi mengi humpata kikiwemo Kifua Kikuu. Lakini si lazima anayeugua Kifua Kikuu awe na Ukimwi.

Hapa Kenya, mojawapo ya mambo yanayochangia kwa kiwango kikubwa maambukizi ya TB ni watu kuwa kwenye mazingira yenye hewa isiyotosha. Ndani ya maduka ya jumla katika miji mingi, orofa za chini au juu hushuhudia msongamano wa wateja, lakini madirisha huwa machacho au wakati mwingine hayapo.

Ndani ya magari ya usafiri wa umma, abiria huamua kufunga vioo kwa kuhofia wachomozi ambao hunyakua simu au bidhaa nyingine za thamani kupitia madirishani.

Japokuwa wananchi wana jukumu katika suala hili, ipo haja kwa viongozi wa ngazi mbalimbali kuunga mkono juhudi za maafisa wa afya kuhamasisha raia kuhusu hatari ya kutokuwa na mzunguko wa kutosha wa hewa safi.

Kwa hivyo, kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni ‘Viongozi Wahitajiwa: Ili kuwa na Ulimwengu bila TB’ yafaa kuzingatiwa na viongozi wote, bila kujali tabaka au uwakilishi wao katika jamii.

Viongozi wan auchawishi mkubwa kwa wananchi. Tungependa kuona MCA, chifu, mzee wa kijiji, viongozi wa vijana na hata rais wa Jamhuri ya Kenya wakijitokeza na kuwaeleza wananchi madhara ya kutozingatia kanuni za kukabiliana na kusambaa kwa TB.

Kwa mfano wanapaswa kuhamasisha watu kwamba wakati mtu anakohoa katika eneo la umma, awe akiziba mdomo kwa kuwa vidudu vinavyosababisha TB hurukakupitia hewa tunayovuta.

Ni kupitia juhudi za pamoja tu, ndipo tutaangamiza Kifua Kikuu.